Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RPC atuma kikosi kazi kijijini kwa agizo la RC

12308 Pic+kikosi TanzaniaWeb

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei ametuma kikosi kazi cha askari kwenda Kijiji cha Ngole kufanya msako na kuwatia nguvuni wananchi waliohusika na uharibifu wa miundombinu ya maji ya Kijiji cha Mashese.

Vijiji hivyo vinavyopakana vipo katani Ilungu wilayani Mbeya na hadi jana jioni hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila alilotoa juzi kwenye kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Chalamila aliagiza wananchi wote waliohusika na uharibifu wa miundombinu hiyo wakamatwe baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wanakijiji wa Mashese kwamba imeharibiwa na watu wa Kijiji cha Ngole.

Akizungumza na Mwananchi jana jioni, Kamanda Matei alisema, “Nimetuma kikosi kazi kwenda kufanya msako na kuwakamata wote watakaobainika kuhusika na uharibifu huo. Tunafanya hivi ili iwe fundisho lakini jioni hii bado sijapata mrejesho wa hatua iliyofikiwa kwa kuwa kule ni mbali, vilevile kuna shida ya mawasiliano. Hivyo vuta subira nitakupa majibu kamili nitakapokuwa nimepewa taarifa kamili.”

Juzi, Chalamila aliagiza wote waliohusika wakamatwe hata ikiwa ni kijiji kizima na wapelekwe gerezani wakafanye kazi na baadaye walipe faini ya uharibifu walioufanya.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mashese, Osia Mwakalila ameieleza Mwananchi kuwa, Agosti 14 wananchi kijijini hapo walikuwa wakiendelea na ujenzi wa chanzo cha maji kutoka hifadhi ya msitu wa Ilungu kwenda kwenye makazi ya watu lakini ghafla maji yalikatwa.

“Tulipofuatilia kujua ni kwa nini maji hayaji kijijini, tuliona kundi la watu wakiwa na silaha na ni wa Kijiji cha Ngole. Tulishauriana tusifanye jambo lolote bali tuondoke,” alisema.

Alisema mipira ya maji ilikatwa na chanzo cha maji kilivunjwa licha ya kuwa hakipiti kwenye kijiji hicho cha jirani.

Alisema waliamua kwenda ngazi ya juu serikalini ndipo juzi walikwenda kwa mkuu wa mkoa Chalamila walikowasilisha malalamiko yao.

Mwakalila alisema mkuu wa mkoa aliwaeleza wasubiri watapatiwa uamuzi wa namna ya kutatua jambo hilo.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngole, Bosco Tayari alisema hakuwa akifahamu kwamba kuna uharibifu umefanywa na wananchi kwenye chanzo cha maji cha wananchi wa Mashese.

“Ninachofahamu huku kwetu kuna migogoro ya ardhi. Vijiji hivi viwili vimekuwa na migogoro ya ardhi tangu enzi za mababu tena eneo lenyewe ni dogo. Hili nalo linachangiwa na mgogoro wa mababu zetu ndiyo unahamia hadi kwa kizazi cha sasa,” alisema.

Alisema jana asubuhi alipata taarifa kwamba askari walipita kijijini hapo wakielekea eneo kunakodaiwa uharibifu wa miundombinu umefanyika.

Tayari alisema hakuna mwananchi aliyekamatwa hadi jana jioni.

Diwani wa Ilungu, Christopher Njerenje alisema anahisi suala hilo ni mwendelezo wa uhasama unaotokana na migogoro ya ardhi ya miaka mingi inayochangiwa na ukosefu wa elimu.

Alisema vijiji hivyo viwili vimekuwa na ugomvi wa mipaka ya eneo la ardhi ambalo dogo.

Chanzo: mwananchi.co.tz