Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RPC abanwa kortini kuzuia kukamatwa basi lililoua

KITINKWIII WEBB Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi.

Wed, 29 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi ameahidi mahakamani atatoa ushirikiano kukamatwa basi la Kampuni ya Mabasi ya Kilimanjaro lenye namba T 178 EAU, ambalo alitoa rukhsa liendelee na safari wakati lilikuwa limekamatwa na dalali wa mahakama.

Kitinkwi alifika juzi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kupata wito wa mahakama ili ajieleze kwanini alikiuka amri ya mahakama ya kukamatwa basi hilo lililotakiwa liuzwe ili familia ya Leonard Kisena ilipwe fidia baada ya kusababisha kifo cha Immaculate Kisena (16) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tano.

Msajili Sundi Fimbo wa mahakama hiyo, alimtaka kamanda wa polisi huyo ajieleze kwanini alifanya hivyo, naye alidai kuwa alipokea simu kutoka kwa abiria akilalamika kuzuiwa kuendelea na safari eneo la Shekilango, Dar es Salaam.

Alidai kuwa kibinadamu alitoa rukhsa waendelee na safari kwa sababu kupata basi lingine kwa wakati huo ilikuwa ngumu.

"Kwa sababu magari huwa yanakaguliwa kabla ya kuanza safari, nikaona kuruhusu gari lingine ambalo halijakaguliwa ingeleta shida, nikaruhusu liende halafu siku iliyokuwa inafuata (Mei 16, 2024) saa saba mchana basi hilo lipelekwe Kituo cha Polisi Oysterbay," alidai RPC Kitinkwi

Baada ya kueleza hayo, kamanda huyo aliahidi atatoa ushirikiano kukamatwa kwa basi hilo na kurudishwa kwa dalali wa mahakama ambaye ni Daniel Mbuga wa Legit Auction Mart.

Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Rolinda Sawaya alipoulizwa na mahakama kama alihusika kuzuia basi hilo, alidai kuwa hakuzuia na hajui mambo ya sheria.

Mkurugenzi huyo tangu shauri hilo lilipofunguliwa, hakuwahi kufika mahakamani hadi alipoandikiwa hati ya kukamatwa.

Baada ya hayo, Msajili Fimbo alitoa amri kuwa utekelezaji uendelee, magari yenye namba za usajili T 178 EAU na T 508 DDB yakamatwe na yakishakamatwa dalali awasilishe mrejesho mahakamani ili kupata ruhksa ya kuyauza. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 3 mwaka huu.

Wakili wa Wadai hao, Mngumi Samadani, nje ya mahakama, alidai kuwa mahakama hiyo ilifikia hatua hiyo baada ya kuwasilisha hoja mahakamani kutokana na dalali wa mahakama kuzuiwa kukamata gari wakati tayari mahakama ilishatoa amri.

Wadaiwa katika shauri hilo namba 47 la mwaka 2022 ni Kampuni ya Kilimanjaro Truck Ltd, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Rolinda Sawaya na Mjahidi Mohamed aliyekuwa dereva wa basi lililosababisha ajali lenye namba za usajili T 278 ALQ aina ya Scania.

Awali akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Jaji Leila Mgonya, Msajili wa Mahakama Kuu, Joseph Luambano alisema wadaiwa wote wanatakiwa kulipa fidia ya Sh. milioni 300 kwa kusababisha kifo, majeruhi na uharibifu wa gari.

Jaji huyo pia alisema watakapochelewesha malipo hayo watatakiwa kulipa riba ya asilimia saba kila siku kwa mwaka na pia wadaiwa watatakiwa kulipa gharama za kesi hiyo; haki ya rufani ipo wazi.

Kisena alifungua kesi hiyo ya madai namba 47, 2022 baada ya kupata ushindi katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani ambayo ilimtia hatiani Mjahidi katika kesi ya trafiki kwa kukiri kuendesha gari hilo bila kuwa na bima, kusababisha kifo, majeruhi Omenis Kabora na uharibifu wa gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 323 CWB.

Kisena ambaye ni baba wa marehemu Immaculate, Desemba 24, 2021, akiwa na watoto wake wawili na mke wake walikuwa safarini kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Alisema walipofika eneo la Kamala Bagamoyo saa 10:15 alfajiri, basi la Kilimanjaro liliacha njia na kuwagonga, ajali iliyosababisha kifo cha Immaculate papo hapo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live