KAMANDA wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani Mkoa wa Mwanza (RTO), Joyce Kotecha amewataka madereva wa mabasi ya mikoani kuhakikisha wanafuata sheria na utaratibu wa nchi yetu.
Hayo alisema jana wakati wa mgomo wa mabasi wa usafiri wa mikoani katika stendi mpya ya mabasi ya Nyegezi mkoani hapa.
‘’Kweli jana asubuhi kulikuwa na sintofahamu lakini baada ya kukaa kikao na wamiliki wa mabasi pamoja na madereva tukawa tumeelewana na tukawapa maelekezo ya Serikali’’ alisema Kotecha.
Alisema baadhi ya kampuni za mabasi zilileta ubishi lakini baadhi yao wamekubali kupeleka abiria. Alisema mgomo ulikuwepo tokea alfajiri saa 10 asubuhi lakini uliisha muda wa saa moja asubuhi.
Aliwaonya wamiliki wa mabasi wasifuate mambo ya kuambiwa na makondakta au maajenti bali wafuate utaratibu na masharti ya usafirishaji.
Mwakilishi wa kampuni ya Allys Star,Said Nasor alikiri kuwepo kwa mvutano kati ya mamlaka ya usafirishaji wa nchi kavu na madereva wa mabasi makubwa kisa ukataji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki.
Alisema kampuni yao haikugoma iliendelea kutoa huduma kama kawaida yao.