Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RPC Manyara awataka wananchi waweke ulinzi kwenye sikukuu

Polisi Pic Benjamin Kuzaga

Fri, 24 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Jeshi la polisi mkoani Manyara limewataka wananchi waweke ulinzi majumbani mwao ili kujilinda wakati huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, huku pia jeshi hilo likiimarisha ulinzi huo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi (ACP) Benjamin Kuzaga, ameyasema hayo mjini Babati Desemba 24 wakati akielezea mikakati ya ulinzi wa polisi kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka.

Kamanda Kuzaga amesema katika kuelekea kwenye sikukuu za Christmas na mwaka mpya, pamoja na polisi kuwalinda watu wajitahidi kuwa walinzi wa mali zao wenyewe.

Amesema jukumu la ulinzi wa raia na mali zake siyo wa polisi pekee ni la jamii kwa ujumla hivyo wananchi nao wahakikishe wanaimarisha ulinzi majumbani mwao.

Pia, amewataka kutokaribisha ovyo watu majumbani ambao ni wageni wasiowafahamu kwani wengine ndiyo wanageuka kuwa wezi wa majumbani.

Amesema wasiwaache watoto peke yao majumbani wao kisha wakaondoka kwenda katika majumba ya starehe bila kuweka ulinzi, kwani siyo jambo zuri kiusalama.

Amewataka wanaotumia vyombo vya moto barabarani wachukue tahadhari kipindi hiki kwa kutoendesha kwa mwendo kasi na kutosababisha ajali.

"Jeshi la polisi tumejipanga kuhakikisha tunawachukukia hatua kali wale wote watakaokuwa wanatumia kwa uzembe na kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa," amesema kamanda Kuzaga.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz