Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC mstaafu adai fidia Sh200 milioni

Rc Moro RC mstaafu adai fidia Sh200 milioni

Wed, 6 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa mkoa mstaafu wa Morogoro, Erasto Sanare amemfikisha mahakamani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Isaac Joseph (Kadogoo), akimtuhumu kumkashifu na kumtolea matusi huku akitaka alipwe fidia ya Sh200 milioni.

Sanare ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Monduli, ameingia katika mgogoro huo kutokana na kuibuka kwa mgogoro wa ardhi baina ya taasisi yake binafsi na halmashauri.

Kesi hiyo ya madai namba 23/2022, ilianza kusikilizwa Ijumaa ya wiki iliyopita mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Aisha Ndossy na Sanare anawakilishwa na mawakili, Kapimpiti Mgalula na Judith Reuben, huku Joseph akiwakilishwa na mawakili Peres Parpai, Sendeu Nicolas na Yonas Masiaya.

Joseph anadaiwa kutoa maneno ya kashfa Novemba 7, 2022 akiwa Sinoni wilayani Monduli akiwa na watu wengine pamoja na waandishi wa habari.

Anadaiwa kusema: “Ndugu yangu Sanare amejiongezea eka moja na pointi kwenye eneo ambalo hajapewa..huu ni wizi imekuwa mambo ya kujirudiarudia sana kwa kiongozi huyu.”

Akitoa utetezi wake mahakamani hapo, Joseph alikanusha kumtukana mkuu huyo wa mkoa mstaafu ambaye ni mkazi wa Monduli.

Akiongozwa na mawakili wake, alisema akiwa kwenye eneo la mgogoro linalomilikiwa na taasisi ya Nanina ambayo Sanare ni mkurugenzi, alitoa maagizo kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo aiandikie barua taasisi hiyo isitishe kufanya maendeleo yoyote kwenye eneo hilo.

Alidai kuwa alifikia uamuzi huo baada ya yeye na timu aliyokuwa nayo ambao walielekezwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Frank Mwaisumbe kupima eneo hilo kujiridhisha kuwa taasisi ya Nanina imejiongezea eneo kama malalamiko ya wananchi na diwani wa eneo hilo wanavyodai.

"Siku hiyo hapakuwa na wananchi, ni wataalam, eneo la mgogoro upande mmoja eneo la Nanina na upande mwingine ni eneo la halmashauri," alisema na kuongeza:

“Sikuwa na chombo cha habari kwenye eneo hilo kwa sababu ili chombo hiki kinachotajwa kuwa nilikuwa nacho kitambulike, lazima kiwe kimesajiliwa na mlalamikaji kwa sasa ni mwananchi wa kawaida sijui kama ni kiongozi wa mila," alidai mshtakiwa.

Alieleza majukumu yake kama mwenyekiti wa halmashauri, ni kusimamia baraza la madiwani, kukagua shughuli za maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Aliieleza mahakama hiyo kuwa Novemba 7, 2022 Saa tatu asubuhi, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumba alimuita ofisini kwake na kumuagiza afuatilie kero ya mgogoro wa ardhi.

"Nilipofika ofisini kwa DC ofisini nikawakuta wataalam wa ardhi na taasisi nyingine Takukuru na polisi. DC wa wakati huo alinieleza kero aliyosema ni ya muda mrefu tukajiridhishe juu ya kero ya eneo tuliyoipa taasisi ya Nanina iliyopo Sinoni kata ya Engutoto," alisema.

Hata hivyo, Sanare alisema licha ya Mwenyekiti huyo wa Halmashauri kumtolea lugha chafu, aliendelea na kazi ya upimaji bila kutoa taarifa.

Hakimu mkazi, Ndossi aliliahirisha shauri hilo mpaka Septemba 15, 2023 kwa ajili ya kutoa uamuzi, huku akiwaagiza mawakili wa pande zote kuwasilisha hoja za majumuisho Septemba 13, 2023.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live