Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC kuwapa zawadi washindi la 7 mil 10/-

E543143784c1b83a086cad611c613b7b.jpeg RC kuwapa zawadi washindi la 7 mil 10/-

Wed, 25 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera ameahidi kutoa Sh milioni 10 zikiwa ni zawadi kwa shule na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu.

Akizungumza mjini hapa, Homera amesema mkoa unatarajia kuandaa sherehe kuwapongeza wanafunzi na walimu kwa kuuwezesha kushika nafasi ya nne kitaifa ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kuwa katika 10 bora kwenye mtihani huo.

“Wakati nimeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi nilikuta mkoa umeshika nafasi ya tisa kitaifa, mwaka 2019 niliupaisha hadi nafasi ya tano mwaka huu umeshika ya nne nikuhakikishie mwakani lazima tutashika nafasi ya kwanza kitaifa,” alisema.

Homera alisema katika matokeo ya mwaka huu mkoa huo umepata ufaulu wa asilimia 91.06 na kwamba sherehe ya kuzipongeza shule na wanafunzi inatarajiwa kufanyika mapema mwakani mjini Mpanda.

“Mkoa kupata matokeo mazuri kitaifa hakuna mchawi mwingine ni motisha kwa walimu na wanafunzi...utaratibu wangu ni kwamba kila alama A ya somo la Sayansi nainunua kwa Sh 20,000 huku A ya Arts ni shiling 10,000. Pia halmashauri kupitia mifuko ya elimu inatoa motisha kati ya Sh milioni mbili hadi tatu kwa mwalimu mmoja,” alisema mkuu wa mkoa.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, katika sherehe hiyo watachinjwa ng'ombe watatu na pia walimu, wanafunzi na shule zilizofanya vizuri watapewa zawadi.

“Mwaka jana kwa kutumia pesa zangu za mfukoni niliwazawadia Sh milioni kumi wanafunzi, walimu na shule zilizofanya vizuri pia kwa hawa wa mwaka huu nitawafanyia hivyo hivyo nitatoa shilingi milioni kumi zangu mie binafsi kama mkuu wa mkoa,” alisema Homera.

Alisema mkoa huo umeshika nafasi ya nne kitaifa kwa kuwa baada ya likizo ya dharura iliyosababishwa na kuenea virusi vya corona wanafunzi wa darasa la saba waliwekwa kambini kwa mwezi mmoja wakilala shuleni na kujisomea.

“Wakati wanafunzi hao wakiwa kambini, nilimkabidhi Ofisa Elimu Mkoa wa Katavi, Newao Mkisi nakala za mitihani ya majaribio "mock" na pre-national examinations niliyoikusanya kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ambayo aliisambaza shuleni na wanafunzi walipewa kuifanya...hadi sasa bado nina nakala za kutosha,” alisema.

Alisema pia wazazi walikubaliana kuchangia chakula shuleni hivyo kupunguza utoro wa kawaida na utoro sugu na kuwezesha wanafunzi wawe na mahudhurio mazuri na wasikivu darasani.

Chanzo: habarileo.co.tz