Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC kicheko ubora miradi ya maji

D9d73816adba0455730451b2c152becf RC kicheko ubora miradi ya maji

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tabora Dk Philemon Sengati amefurahishwa na ubora wa miradi ya maji iliyotekelezwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Tabora.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama uliotekelezwa katika kijiji cha Migungumalo kata ya Usagari wilayani Uyui juzi alimpongeza Meneja wa Ruwasa Mkoa kwa usimamizi bora wa miradi.

Alisema kuwa miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali mkoani humo imeongeza kiwango cha upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijijini kutoka asilimia 30 hadi 70.

'Nimeridhishwa na utendaji wa Ruwasa katika mkoa huu, endeleeni hivi hivi, naamini miradi hii na ule wa ziwa Victoria uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 600 itamaliza kero ya maji katika wilaya zote saba za mkoa wetu', alisema.

Sengati alibainisha kuwa weledi na ufanisi wa wataalamu hao umewezesha mkoa huo kuongoza nchi nzima katika utekelezaji miradi ya maji iliyogharamiwa na mradi wa P4R.

Alifafanua kuwa mahitaji ya maji katika mkoa huo ni lita za ujazo milioni 37 wakati yaliyozalishwa kutokana na mradi mkubwa wa ziwa Victoria ni lita milioni 54 hivyo kuufanya mkoa huo kuwa na maji mengi kuliko watumiaji kwa maeneo ya mjini.

Alieleza kuwa huduma ya maji safi na salama imeboreshwa kwa kiasi kikubwa katika mkoa huo kutokana na usimamizi bora wa miradi iliyotekelezwa hivyo akatoa wito kwa wageni kuja kujifunza kupitia miradi hiyo.

Sengati aliwataka wakazi wa mkoa huo kujiepusha na vitendo vya uharibifu wa mazingira ili kulinda na kutunza vyanzo vya maji vilivyopo.

Meneja wa Ruwasa mkoani humo Hatari Kapufi alisema kuwa hadi kufikia Machi, mwaka jana wakazi milioni 1.47 kati ya milioni 2.39 waishio vijijini walikuwa na uwezo wa kupata huduma ya maji safi kwa asilimia 62.4 kwa baadhi ya maeneo asilimia imeongezeka hadi 70.

Alibainisha kuwa RUWASA imetekeleza miradi mbalimbali mkoani humo kupitia programu za PbR, P4R na Mfuko wa Maji (NWF) .

Aliongeza kuwa kupitia mpango huo jumla ya miradi 31ya maji yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 8.7 imetekelezwa katika mkoa huo na baadhi imekamilika na mingine iko katika hatua za mwisho.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kaliua mkoani hu,o Salome Luhingulanya alisema kuwa serikali ya CCM inawajali wananchi wake hivyo akawataka wakazi wa mkoa huo kutumia vizuri miradi hiyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz