Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC azihoji kampuni za simu wizi mtandaoni

56754 Pic+RC

Mon, 13 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amezitaka kampuni za simu nchini kutunza siri za wateja wao na kuhoji wapi wezi wa kimtandao wanapata namba za mawakala wa huduma za fedha na kuibia wateja.

Akizungumza jana mjini hapa, Dk Mahenge alisema pamoja na juhudi za jeshi la polisi kutuma ujumbe kwa wateja wa mitandao ya simu kuwataka kuwa makini na wezi wa kimtandao, lakini bado kuna Watanzania wanaibiwa.

“Wapo vijana wana namba za mawakala wote wa mitandao ya simu nchini na wanapiga na kuhamisha fedha yaani wanaibia wateja.”

“Hii ina maanisha wawekezaji katika mitandao ya simu wanatakiwa wawekeze kuzuia uhalifu huu kwa kushirikiana na Serikali kudhibiti,” alisema.

“Kwanini mtu awe na orodha ya namba zote za wenye M-pesa ama kampuni nyingine ameipata wapi? Nani kampatia ni kazi ya kampuni za simu kutunza siri za wadau wenu ambao wamekuja kujisajili na kuwapa namba za Tigo Pesa ama M-pesa ili orodha isiende kwa mtu mwingine.”

Mkuu huyo wa mkoa ameitaka kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom PLC ambayo imefungua ofisi na duka jijini Dodoma kuwekeza katika utafiti wa teknolojia ambayo itadhibiti makosa ya kimtandao.

Pia Soma

Kwa upande wake, mkurugenzi wa mahusiano na mawasiliano wa kampuni hiyo, Rosalynn Mworia alisema huduma za mawasiliano ni muhimu katika kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi.

“Tumeona umuhimu wa kuongeza nguvu Dodoma kwa kufungua ofisi zetu na pia kuongeza duka jipya, nia yetu ni kuchochea shughuli za kiuchumi za mkoa huu,” alisema.

Naye Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alisema kampuni ya Vodacom ina nafasi kubwa ya kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kupunguza umasikini. “Na mnaweza kufanya vizuri huduma yenu ya Mpesa. Vijana wengi wamejiajiri kwa kuwa na vibanda na mawakala na wengi wangependa kufanya hivyo lakini ukosefu wa mitaji ni kikwazo, niombe muweke utaratibu mzuri wa kuwezesha vijana kupata kianzio cha kufanya kazi hii,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz