Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC aziagiza halmashauri kutoa elimu ya corona

89992c963bc4faf94067c0111cf6cf1b.jpeg RC aziagiza halmashauri kutoa elimu ya corona

Thu, 15 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Balozi Wilbert Ibuge ameziagiza halmashauri nane katika mkoa huo kupitia wataalamu wa afya zisimamie elimu ya kujikinga na maambukizi ya wimbi la tatu la corona.

Balozi Ibuge alitoa agizo hilo alipozungumza na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watumishi wa umma ngazi ya mkoa na wilaya kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Songea.

Aliagiza kuwe elimu endelevu ya kujikinga kabla ya kuugua corona itolewe kwa wananchi ikiwemo kuvaa barakoa, matumizi ya kunawa kwa sabuni na maji titirika na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.

“Nimepita na kuzunguka baadhi ya maeneo mjini Songea nimeona wananchi wameacha zile hatua ambazo tulikuwa tumezichukua katika wimbi la kwanza mfano, nje ya maeneo ya huduma ndoo hazina maji wala sabuni, tukasimamie kuwaelimisha wananchi kwa sababu kujikinga ni gharama ndogo kuliko kutibu,” alisema Balozi Ibuge.

Alisema corona ipo nchini, lakini katika mkoa huo tishio si kubwa, lakini kwa kuwa kuna mwingiliano wa watu kusafiri na kuingia na kutoka elimu ya kujikinga isimamiwe.

“Suala la kujikinga ni rahisi kuonekana halina umuhimu kama madhara bado hatujayaona, sote tumekuwa tukisikia maelekezo mbalimbali kutoka Wizara ya Afya na kupitia viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wimbi la tatu la corona tayari lipo nchini tuchukue tahadhari,” alisema Balozi Ibuge.

Chanzo: www.habarileo.co.tz