Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC atoa wiki familia 10 zihame Bonde la Wembere

7c9620b85937b28a135d0c4a86231b69 RC atoa wiki familia 10 zihame Bonde la Wembere

Mon, 19 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati ametoa siku saba kwa familia 10 za wafugaji na wakulima zihame kutoka Bonde la Wembere wilayani Igunga.

Dk Sengati alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara katika eneo hilo kukagua utekelezaji wa agizo la kuwataka watu waliokuwa ndani ya bonde hilo waondoke kwa hiyari.

Alisema hadi sasa zaidi ya familia 200 zimehama kwa hiyari katika eneo hilo na kwenda katika eneo maalumu walilopangiwa, lakini 10 zimeendelea kubaki.

Dk Sengati alisema katika mkutano uliofanyika katika kijiji cha Makomero mwezi uliopita, walikubaliana familia 13 kati ya 200 zilizokuwa ndani ya bonde hilo ziondoke, lakini 10 kati ya hizo zimeendelea kukaidi.

Alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo kwa kushirikiana na polisi wa wilaya hiyo wamtafute kiongozi wa kundi la wakulima na wenzake wawili wanaodaiwa kuhamasisha wenzao wasiondoke kwenye eneo hilo.

"Hizi kaya 10 zilizobaki ndani za siku 7 ziondoke ili serikali iweze kutekeleza majukumu yake katika eneo hili, ndani za siku saba sitarajii kuzikuta kaya hizi zikiwa bado ndani ya bonde hili,” alisema.

Dk Sengati alisema hatarajii kuona wanasiasa wanatumia siasa katika eneo hilo ambalo lina maslahi kwa maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa Tanzania si kisiwa na imeridhia mikataba ya kimataifa ikiwamo ya kutunza na kuhifadhi maeneo oevu.

Alisema eneo hilo ni mali ya serikali na lina maslahi kwa nchi ukiwamo utafiti wa gesi na mafuta na ni chujio la maji yanayokwenda Ziwa Eyasi.

Dk Sengati alitaja maslahi mengine kwenye eneo hilo kuwa ni uwepo wa ndege aina ya flamingo ambao wanapatikana maeneo machache duniani na bonde hilo ni njia ya wanyamapori wanaokwenda pori la akiba la Rungwa.

Alisema ofisi yake itafanya majadiliano na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Nishati, Wizara ya Maji na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ili waainishe eneo ambalo lina maslahi kwa nchi na litakalobaki wapewe wananchi kwa utaratibu mzuri.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga (OCD), Ally Mkalipa alisema Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Igunga ilikwenda katika eneo hilo na kufanya kikao na wananchi na walikubali kuhamia katika eneo walilolipenda.

Mkalipa alisema kitendo cha familia 10 kuendelea kubaki hapo ni ukaidi na zinakiuka makubaliano hivyo watachukua hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Alisema familia hizo zinatumia mbinu za wanaume kujificha mchana na kuacha watoto na wanawake na ikifika usiku wanarudi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz