Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC atoa tamko anayetuhumiwa kumkata masikio mpenzi wake

Newslite1640938624003 RC atoa tamko anayetuhumiwa kumkata masikio mpenzi wake

Sun, 2 Jan 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani hapa kumsaka na kumtia nguvuni Nyang’oso Chacha, anayetuhumiwa kumkata masikio mpenzi wake, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Mkirikiti ametoa agizo hilo leo, wakati akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu uliofanyika katika viwanja vya Nelson Mandela mjini hapa.

“RPC yuko wapi?...sasa nakuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga waeleze polisi popote alipo Chacha akamatwe, nasikia yeye ndio bingwa wa kukata watu masikio na kuna malalamiko mengi dhidi yake, huu sio utawala wa kuchezea chezea watu,” aliagiza.

Alisema kuwa hatakubali kuona mabucha ya Chacha yakifanya kazi ya kuuza nyama wakati yeye anaripotiwa amekimbia na hajulikani alipo... “Sasa atafutwe popote alipo ndani ya nchi hii na akamatwe ili sheria ichukue mkondo wake,” alisisitiza.

Kauli ya Mkuu huyo wa mkoa, imekuja siku chache baada ya kutokea tukio la Dorcas Richard (23) kukatwa masikio na mwanamume kwa madai ya wivu wa mapenzi.

Pia, ndugu wa mwanamke huyo, wananchi na wanaharakati wa kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia pamoja na kulaani vikali kitendo hicho, wamepaza sauti wakitaka Chacha akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.

Pamoja na kulaani, pia wamelitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa kumsaka na kumtia nguvuni Nyang’oso Chacha, anayetuhumiwa kufanya ukatili huo.

Ndugu wanena

Mjomba wa Chacha, aitwaye Isaya Anzuri alisema kitendo cha mpwa wake kumkata mwenzake masikio ni ukatili uliopitiliza na haukubaliki, hivyo sheria lazima ichukue mkondo wake.

“Hili tukio haliwezi kuvumilika, ni hatua ya mauaji, kwani kumkata mwenza wako masikio na kuondoka nayo anamaanisha nini?” alisema na kuhoji Anzuri.

Majirani wanasemaje?

Mmoja wa majirani wa Chacha, Salma Said, mkazi wa Majengo mjini hapa, alisema anashangaa kwa muda mrefu kijana huyo amekuwa akifanya vitendo vya ukatili dhidi ya wake zake pasipo kuchukuliwa hatua za kisheria, badala yake kesi zake zinamalizwa chinichini na polisi pasipo kufikishwa mahakamani.

“Huyu mtu utafikiri yupo juu ya sheria, anawafanyia sana ukatili wake zake...Kuna mmoja alimpiga hadi kumvunja miguu lakini hata mwanamke huyo alipolalamika suala hilo liliisha kimya kimya, sijui anajivunia nini?” alihoji.

Taasisi zatoa tamko

Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya wanawake 100,000, Marry Goreth Matondwa alisema kuwa Chacha akamatwe na ikibainika anahusika achukuliwe hatua.

Aliyekatwa masikio aelezea mkasa ulivyotokea

Kwa upande wake, Dorcas, mkazi wa kitongoji cha Bible mjini hapa, aliyekatwa masikio yake yote mawili usiku wa kuamkia Desemba 28, 2021 akiwa nyumbani kwake, alisema kwamba tukio hilo lilitokea saa tano usiku ikiwa ni muda mfupi baada ya Chacha kuingia nyumbani hapo na kumnyang’anya simu ya kiganjani kisha kuanza kuipekua, kisha kumwambia “Kwa nini unanisumbua, sasa nakukata masikio ili hao wanaokufuata fuata waache”.

Baada ya kueleza hivyo, inadaiwa mwanamume huyo alimtaka ainame ili aanze kumkata sikio moja baada ya jingine ambapo alimkata sikio moja kisha la pili huku mwanamke huyo akigugumia maumivu.

Alisema baada ya tukio hilo aliishiwa nguvu kutokana na kutokwa na damu nyingi. “Alinichukua na kunipeleka hospitali na kuondoka, nikatundikiwa chupa tatu za maji .

“Aliondoka na yale masikio na kusema nisijaribu kutoa taarifa polisi kwa sababu hawatamfanya chochote, nimeishi naye miaka mitatu mambo ni haya nisiende hata kusalimia ndugu, ana wivu sana,” alisema Dorcas.

Kauli ya Jeshi la Polisi

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna msaidizi wa Polisi, Mashenene Mayira alisema wanaendelea na jitihada za kumtafuta mtuhumiwa huyo ili wamfikishe kwenye vyombo vya sheria.

“Mimi ni mgeni mkoani hapa, sina taarifa za matukio yake mengine ya kunyanyasa watoto na wake zake, ila tutakapomkamata yote hayo yatajulikana, kwa sasa jitihada zilizopo kwanza ni kumkamata,” alisema Mayira.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz