Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC atoa siku 90 kiwanda kizalishe sukari

7f3bec1a088a540ec0e4279c1c83057b RC atoa siku 90 kiwanda kizalishe sukari

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa (RC) wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ametoa siku 90 kwa mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari cha Purandare Sugar Production Limited kilichopo wilayani Chamwino, Dodoma kuanza uzalishaji.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo ambalo kiwanda hicho kinatakiwa kujengwa katika Kijiji na Kata ya Dabalo katika Wilaya ya Chamwino, Mahenge alisema mwekezaji huyo Satesh Purandare anatakiwa kuanza uzalishaji ndani ya muda huo ukimalizika, halmashauri itafute mwekezaji mwingine.

Alisema mwekezaji huyo amekuwa akipiga danadana kwa kuleta visingizio na kukwamisha uzalishaji licha ya kutekelezewa maombi yake yote kwa kisingizio cha vifaa kukwama India kutokana na kuibuka kwa ugonjwa wa covid-19, barabara mbovu na umeme, sababu alizosema hazina ukweli.

Kwa upande wake, mwekezaji huyo Satish Purandare, alisema wamekwama kuanza ujenzi wa kiwanda kutokana na ugonjwa wa covid-19 kuzuia kukwamisha usafirishaji wa vifaa sambamba na ubovu wa barabara na ukosefu wa umeme mambo yaliyochangia kuchelewesha kuanza ujenzi na uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho.

Purandare aliahidi kuwa, kabla ya Februari mwakani, wataanza ujenzi wa kiwanda na kuanza uzalishaji wa sukari utakaoanza kwa kutoa ajira 500 za moja kwa moja na ajira 1,000 za kihuduma, 1,000 kwa wananchi wa vijiji vya Dabalo, Igamba, Nayu, Ikombo na Manyemba.

Akizungumiza kuchelewa kwa ujenzi na uzalishaji sukari katika kiwanda hicho, Mahenge alikitaka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kanda ya Kati, kutomwongezea muda mwingine mwekezaji huyo kama walivyofanya mara ya kwanza kwa kumpa mwaka mmoja utakaomalizika Februari mwaka ujao, lakini kiwanda hakijengwa wala kuanza uzalishaji.

Alisema baada ya mwekezaji huyo kupata vibali vyote vya kumiliki ardhi, uzalishaji na vyote vinavyostahili, hadi sasa hajaonesha nia ya kuanza uwekezaji katika muda wote aliopewa kuanza uzalishaji.

Dk Mahenge aliwataka wananchi wanaolima miwa kwa ajili ya kulisha kiwanda hicho kitakachojengwa kuendelea kuwa wavumilivu.

Mkurugenzi wa TIC Kanda ya Kati, Abubakar Ndwoto, alisema atamwita mwekezaji huyo ofisini kwake kumhoji kama ana dhamira ya dhati ya kuwekeza, lakini pia kituo hakitaongeza muda mwingine.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino, Athuman Masasi alisema halmashauri hiyo imeonesha ushirikiano na mwekezaji huyo kwa kumpa kila mahitaji aliyotaka kuanza uzalishaji, lakini hajaanza uzalishaji.

Alisema muda aliotoa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ukiisha kabla hajaanza uzalishaji, wapo tayari kuanza mchakato wa kumtafuta mwekezaji mwingine.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga, aliwapongeza wananchi wa Kijiji cha Dabalo katika Kata ya Dabalo wilayani Chamwino kwa kuvumilia kwa muda wote wakisubiri mwekezaji kuanza kuzalisha sukari na kuendelea na uzalishaji wa miwa kwa ajili ya kiwanda hicho.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Dabalo, Omari Kiguna, aliishukuru Bodi ya Sukari Tanzania kwa kuwafidia wananchi 79 wenye mashamba ya miwa yanayofika ekari 1,885 waliolima miwa, lakini kiwanda hakijajengwa na hakijaanza uzalishaji hadi sasa.

Chanzo: habarileo.co.tz