Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC ataka walioiba mashine ya nyama wasakwe

5744836921d04f40d161ca1313e000cc RC ataka walioiba mashine ya nyama wasakwe

Thu, 22 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa (RC) wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Dodoma, Gilles Muroto kuwasaka walioiba mashine ya kuchakata nyama na mota ya kusukuma maji katika Kiwanda cha S&Y Gurment Meat Product Limited.

Kutokana na kuibwa kwa mashine hizo, tangu mwaka jana kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchakata ng'ombe 200 na mbuzi 1,000 kwa siku kimesimamisha uzalishaji.

Hali hiyo imesababisha vibarua 120 wa kuchakata nyama na 55 wa kutengeneza vifaa vya mbao katika kiwanda cha S&Y Wood Product Co Limited wamepoteza ajira zao.

Dk Mahenge alitoa maagizo hayo kwenye viwanda hivyo katika maeneo ya Zuzu jijini hapa baada ya kupewa taarifa kwamba, kiwanda cha S&Y Gurment Meat Product Limited kimesimama uzalishaji baada ya mashine ya kuchakata nyama yenye thamani ya Sh milioni 31 kuibwa.

Alimtaka Meneja wa viwanda hivyo, Titus Gembe kuwasilisha nyaraka za utambulisho wa aina ya mashine hiyo iliyoibiwa ofisini kwa RPC ili kuanza kuwasaka wezi popote walipo na kuwatia mbaroni.

Aidha, Mahenge alimtaka RPC Muroto kwenda kufuatilia majalada ya malalamiko manane yaliyofunguliwa polisi na viongozi wa kampuni hizo yakiwemo ya kuwashitaki walinzi na kampuni za Martiz na Jagro ambao mashine na mota zimeibwa wakati wakilinda hata kama hawakuwa na mikataba ya kulinda hapo.

Alimwagiza meneja wa kiwanda hicho na kingine pacha cha S&Y Wood Product Co Limited kuwasilisha nyaraka zinazoonesha mtaji na rasilimali za kampuni hiyo katika ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kanda ya Kati ili ifanye tathmini ya uwezo wake ili kupewa ushauri wa kufufua kiwanda hicho.

Mkuu wa Mkoa aliwataka waendeshaji wa viwanda hivyo Meneja Gembe na rai wawili wa China ambao ni Kaimu Meneja, Jinha Da na Mkurugenzi na mmiliki wa viwanda hivyo aliyepo China, Song Zhichao kuacha kuchukua walinzi wa mitaani kwa kuangalia gharama nafuu.

Alisema walinzi wanaopatikana katika kampuni ambazo hazijasajiliwa kwa gharama nafuu mara nyingi amekuwa wakibainika kusababisha hasara.

Dk Mahenge aliagiza kushirikiana na taasisi mbalimbali na viongozi wa kata akiwamo Diwani wa Zuzu, Awadh Abdallah na Mwenyekiti wa Mazengo, Joshua Kajembe kusaidia kutoa ulinzi.

Alisema viongozi hao wanawajua vijana, hivyo wanaweza kusaidia hata kuwaonya wasijihusishe na vitendo vya wizi katika kiwanda.

Kamanda Muroto aliahidi kuwasaka wezi wa mashine na mota ya kusukuma maji kwenda kiwandani pamoja na kufuatilia kujua hatima ya majalada manane yaliyofikishwa polisi na wamiliki wa viwanda ili kujua kwa nini yamekwama na yamekwama wapi katika ofisi yake.

Alimtaka meneja wa viwanda hivyo Gembe, kuwasilisha ofisini kwake vielelezo vinavyobainisha aina ya mashine ya kuchakata nyama iliyoibwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz