Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC ataka vyumba 148 vikamilishwe haraka

F8c14c720f10a41fb3cbb9b6da31c3e9 RC ataka vyumba 148 vikamilishwe haraka

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa mkoa wa Dodoma Dk Binilith Mahenge ameagiza kila halmashauri kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa madarasa 148 ili wanafunzi zaidi ya 7,000 waliokosa nafasi wapate fursa ya kusoma.

Jumla ya wanafunzi 35,215 walifaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu na waliochaguliwa ni 28,070 wakati 7,145 wakikosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Akizungumza juzi wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa, Dk Mahenge alisema halmashauri zote zihakikishe zinakamilisha ujenzi wa madarasa hayo ili kila mwanafunzi aliyefaulu apate fursa ya kwenda shuleni.

Mkoa wa Dodoma wenye halmashauri nane una jumla ya upungufu wa vyumba vya madarasa 148 wakati jiji la Dodoma likiwa na upungufu wa madarasa 52, Chamwino upungufu wa madarasa 40, Konga 21, Mpwapwa 12, Kondoa DC 10, Chemba 8, Bahi 5 na Kondoa Mji haina upungufu.

Alitaka kila halmashauri kujipanga ili watoto waliripoti shuleni na kuwataka wakurugenzi wa halmashauri, wenyeviti wa halmashauri na wakuu wa wilaya kuhakikisha suala la kukabiliana na upungufu linakuwa ajenda ya kudumu na si kusubiri mpaka wanafunzi wachaguliwe.

Ofisa elimu Mkoa wa Dodoma, Maria Lyimo alisema mkoa una shule za sekondari za serikali alisema mahitaji ni vyumba 704 kwa uwiano wa 1:50 na hali halisi ya vyumba vilivyopo ni 536.

Alisema changamoto zilizopo katika mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2021 ni pamoja na upungufu wa miundombinu na samani za shule, vyumba vya madarasa, madawati, muza na viti na baadhi ya shule kuwa mbali na makazi ya jamii hivyo wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Mkurugenzi wa wilaya ya Bahi, Dk Fatma Mganga alisema inapofika kwenye suala la elimu kila mmoja anatakiwa kuwa makini ili kuongeza kiwango cha ufaulu.

Alisema mwaka huu Bahi imeshika nafasi ya kwanza ya ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba wakiwa na asilimia 84.64 na nafasi ya 83 kitaifa lakini jambo hilo limewezekana kutokana na ushirikiano uliokuwepo kati ya watendaji na walimu.

Chanzo: habarileo.co.tz