Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC ataka madereva walevi waweke rumande mpaka mwaka mpya

Db573d3b7a29e7a136e366067bf01bcd.png RC ataka madereva walevi waweke rumande mpaka mwaka mpya

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa mkoa Arusha, Idd Kimanta ameliagiza jeshi la polisi mkoani humo kukamata madereva wote walevi na kuwaweka ndani kuanzia sasa hadi zitakapopita Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya ili kulinda uhai wao na wa abiria watakaowapakiza.

Kimanta alitoa maagizo hayo jana alipokuwa akihutubia kwenye hafla fupi ya maadhimisho ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yaliyoadhimishwa viwanja vya Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha na Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa huo (TPF NET).

Alisema zimekuwa zikitokea ajali zisizo za lazima siku za sikukuu za mwisho wa mwaka sababu ya watu wachache wasiotaka kufuata sheria za nchi kwa kunywa pombe kupita kiasi na kuendesha vyombo vya moto.

“Sasa hapa mkoani kwangu sitaki ajali za makusudi kuanzia sasa RPC nakuagiza ukikuta dereva kalewa huku anaendesha gari mkamate na asitoke hadi mwaka mpya kwa ajili ya usalama wake ingawa dhamana ni haki ya kila mtu lakini maisha yake ni mali ya serikali,” alisema.

Alisema kumekuwa na tabia ya watu kukamatwa na kuwekwa ndani kisha baada ya siku moja au siku hiyo hiyo mlevi huyo anapewa dhamana, hilo sasa likome na kuongeza kuwa madhara yanayosababishwa na walevi wanaotumia vyombo vya moto ni makubwa kuliko wao kusaidiwa kuhifadhiwa ndani.

Aidha aliomba wananchi kuchukua tahadhai ya kutoacha nyumba zao bila watu kipindi hiki kuelekea sikukuu za mwaka mpya na krismasi.

“Hivi sasa wahalifu wamebadili mfumo wanavunja nyumba mchana na kuiba badala ya usiku sababu ya doria za polisi, sasa nanyi wananchi hakikisheni mnaweka watu nyumbani msitoke wote, japo polisi wataongeza doria mchana na usiku lakini na nyinyi muwe na tahadhari,” alisema.

Kamanda wa Polisi Salmu Hamduni alisema amepokea maelekezo ya mkuu huyo na atayafanyia kazi ili kila mmoja aheshimu sheria za barabarani na sikukuu zipite kwa usalama bila ajali mkoani humo.

Chanzo: habarileo.co.tz