Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC ataka jamii ihusike kukabili mihadarati

843608c553cb52e202fdc3783eff44b6 RC ataka jamii ihusike kukabili mihadarati

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela amesema suala la uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya lisiachiwe vyombo vya ulinzi na usalama tu, jamii nzima ihusike katika kudhibiti vitendo hivyo visiendelee kuwepo nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu huyo wa mkoa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaasha Tumbo jana wakati akizindua mradi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa wilaya za Tanga Jiji na Muheza ulioratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Taasisi ya Casa Famigila Rosetta.

Alisema athari za dawa za kulevya zinakwenda moja kwa moja katika jamii, hivyo kuachia kundi moja pekee kupambana na tatizo hilo hakutaweza kufikiwa kwa malengo ya kumaliza changamoto hiyo.

Alisema ifike mahali iwe ni lazima jamii nayo ishiriki moja kwa moja katika kuwafichua waingizaji wa dawa hizo ili serikali iweze kuwachukulia hatua za kisheria kwa haraka kabla hawajaanza kuuza dawa hizo.

"Niwatake watendaji wa vijiji, mitaa na vitongoji katika hizi wilaya mbili nendeni mkashirikiane na wananchi katika kuwadhibiti na kuwabaini waingizaji wa dawa za kulevya na mtoe taarifa ili waweze kudhibitiwa na vyombo vyetu vya usalama," alisema.

Alisema licha ya serikali kuchukua jitihada kubwa ya kupambana na janga hili lakini kumeibuka changamoto mpya ya baadhi ya watumishi wa afya kuchepusha dawa za hospitali na kuziingiza kinyemela kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

“Hivyo nimuagize Mganga Mkuu wa mkoa wa Tanga kufanya ufuatiliaji na iwapo watabainika wahudumu wa afya ambao wanatumika katika hujuma hiyo kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine,”alisema.

Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Omary Ubuguyu alisema mikoa ya Dar es Salaam na Tanga ndio ambayo imeathirika kwa kiwango kikubwa na dawa za kulevya kwa hapa nchini.

Alisema kitakwimu Dar es Salaam pekee ina waathirika wapatao 150,000 huku mkoa wa Tanga ukiwa na watumiaji zaidi 60, 000 ambao wanatumia dawa aina ya heroini.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Taasisi ya Casa Famigila Rosetta, Irene Kaoneka alisema kutokana na jitihada ambazo zinachukuliwa na serikali wameamua kuziunga mkono ili kuhakikisha wanapambana katika kupunguza au kumaliza tatizo hilo.

Alisema kupitia taasisi yake wameweza kutoa mafunzo ya utambuzi wa viashiria vya matumizi ya dawa kwa ngazi ya jamii kwa watu 45 ambao wapo kwenye jamii ambao watakuwa na kujukumi pia la kutoa elimu juu ya athari za dawa hizo .

Chanzo: habarileo.co.tz