Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela, amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa NHC kufikiria namna ya kuwekeza kwenye mradi wa maduka makubwa (mall) kwa ajili ya kurahisha upatikanaji wa huduma muhimu.
Akizungumza na uongozi wa NHC ulipomtembelea ofisini kwake juzi ukiwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula, wakati wa kikao chake na Jukwaa la Wahariri Tanzania mkoani haoa, Shigela alisema kwa sasa mkoa hauna maduka kwa ajili ya kuwawezesha wakazi kupata huduma eneo moja kama ilivyo Dar es Salaam.
"Morogoro ni mji mkubwa wenye vituo vingi vyenye idadi kubwa ya watu, lakini hakuna ‘supermarket’ kubwa mfano wa mall, hivyo kama Shirika letu la Nyumba mfikirie namna ya kufanya uwekezaji katika eneo hilo," alisema Shigela.
Kwa mujibu wa Shigela, mbali na NHC kuwa na nyumba za makazi katika baadhi ya maeneo, uhitaji wa nyumba pamoja na maduka makubwa bado upo kwa lengo la kuwawezesha wakazi wake kupata huduma.
Alisema kwa sasa Mkoa wa Morogoro unazidi kukua kwa kasi na pia ni njia kuu ya kwenda Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Rwanda na kubainisha kuwa tayari umeanza kuainisha maeneo ya uwekezaji hasa inapopita reli ya mwendokasi.
Naibu Waziri Mabula alisema suala la kujenga ‘mall’ linawezekana, lakini alitahadharisha utekelezaji wake usikwamishe miradi mingine ya shirika kwa kuwa NHC imepewa ujenzi wa ofisi baadhi ya wizara katika mji wa serikali eneo la Mtumba, Dodoma.
"Kujenga ‘supermarket’ kubwa ni jambo la kuangalia na mawazo yachukuliwe ilmradi utekelezaji wa miradi mingine isikwame. Ni lazima mjipange wajipange, wekezeni mpate pesa na biashara ni matangazo," alisema Dk. Mabula.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando, aliuomba uongozi wa NHC kupitia upya gharama za kupangisha nyumba pamoja na kuzifanyia ukarabati ili ziwe na mwonekano mzuri kwa kuwa baadhi zimechakaa.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dk. Maulid Banyani, alimhakikishia Shigela kulifanyia kazi suala hilo na kueleza kuwa shirika limekuwa na mikakati mbalimbali ikiwamo kujenga nyumba maeneo ya pembezoni.
Pia alisema katika kuhakikisha shirika linatekeleza ombi la mkuu wa mkoa wa kuangalia namna ya kufanya uwekezaji wa maduka, lilitembelea kingo za Sabasaba pamoja na Naibu Waziri kuona namna ya kufanya uwekezaji katika eneo hilo.