MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema si sahihi kujenga majengo ya ghorofa kwa ajili ya masoko ya wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga.
Chalamila alisema jana kuwa, Machinga ni wachuuzi hivyo ni vigumu kwa wateja kuacha maduka ya chini na kuwafuata juu ghorofani.
“Kumekosewa sana, kwa asilimia 11, 608, kumekosewa sana” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema si sahihi kwa wafanyabiashara wadogo kuwa na maduka sehemu za juu ghorofani na wafanyabiashara wakubwa kuwa sehemu ya chini kwani Wachinga ni wachuuzi hivyo bei zao ni kubwa kuliko za kwenye maduka ya jumla.
“Kinachotokea ni nini mteja akifika anakwenda kwenye maduka ya jumla ambako vitu vinapatikana kwa bei ya chini sasa atakuwa na sababu gani ya kupanda juu kwenye ghorofa ajichoshe kupandisha juu kwenda kumfuata mchuuzi anayeuza kitu mara mbili ya bei ya muuzaji aliyepo kwenye vibanda vya chini.
“Huhitaji kutumia mabilioni ya fedha kujenga soko la Machinga kwa sababu wafanyabiashara hao hawahitaji maghorofa kwa sababu hata kabla ya kwenda huko wanauza bidhaa mitaani.
“Tumelijenga soko katika miundombinu ya kawaida sana na si miundombinu ya mabilioni ya pesa lakini tulichokifanya tumezuia pia wale madalali wachache ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilialia serikali inapochukua kodi zake,” alisema.