Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC aonya shule zinazofanya udanganyifu wa mitihani

22a9d3be052dce5343506e046549ad9a RC aonya shule zinazofanya udanganyifu wa mitihani

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHULE zinazofanya udanganyifu wa mitihani ili zionekane zinafanya vizuri, zimeonywa na kutakiwa kuacha tabia hiyo mara moja.

Imeelezwa kuwa kufanya hivyo, kunaongeza wasomi wasio na sifa, jambo ambalo linakuwa mzigo kwa taifa.

Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid alisema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Abubakar Kunenge kwenye Mahafali ya Pili ya Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Ihsan iliyoko Wilaya ya Kigamboni. Mahafali hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki na yalihusisha wahitimu 87,

Alisema serikali imejipanga kuondokana na changamoto ya wizi wa mitihani ili kuzalisha wasomi watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

“Vijana wanaohitimu katika shule zote hapa nchini ni wa serikali na wanapokosa ajira lawama zote huenda kwa serikali na sio shule zilizozalisha ufaulu wa kupikwa. Tumejipanga na hatutasita kuchukua hatua kwa shule yoyote ambayo italeta udanganyifu katika mitihani,” alieleza.

Aliipongeza shule ya Ihsan kwa kuwaandaa vizuri vijana katika uadilifu na ucha Mungu na kuwataka vijana waliohitimu, wakawe mabalozi wazuri huko waendako.

“Mbali ya kuwafundisha vijana hawa masomo ya kawaida, lakini kubwa mlilolifanya ni kuwajenga katika uadilifu na ucha Mungu jambo ambalo Taifa litanufaika kwa kuwa na kizazi chenye hofu ya Mungu,” alisema.

Mkuu wa mkoa alisema hakuna namna nyingine ya wanafunzi kufanya vizuri, zaidi ya kuajiri. Alisema walimu wenye sifa na wale wanaoajiriwa kutoka nje ya nchi, lazima wafuate taratibu za uhamiaji.

Mkuu wa shule hiyo, Dk Hashimu Saiboko alisema ataendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi zote za serikali na binafsi ili kwa pamoja waweze kufikia malengo mazuri ambayo serikali imeyaweka.

Alisema kwa sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 400 huku mahitaji ya miundombinu yake ni zaidi ya wanafunzi 600, hivyo aliwataka wazazi kujitokeza kwa wingi kuomba nafasi shuleni hapo.

“Tuna kila kitu kilicho bora ikiwemo madarasa, mabweni, vyumba vya kompyuta, masomo ya elimu ya dini ya Kiislamu na walimu wa kutosha ambapo uwiano wake ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi kumi na tatu (1:13), tunawaomba wazazi waje kuandikisha watoto wao kwa muhula wa 2020/21,” alieleza.

Mbarouk Mansour ambaye ni mhitimu, alisifu jitihada za walimu kwa walivyowajenga na anaamini watakuwa na matokeo mazuri katika mitihani ya kidato cha nne, iliyomalizika mwisho mwa wiki.

Chanzo: habarileo.co.tz