Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC aonya polisi wanaodai rushwa kwenye baa usiku

De9759b0a1080064f14649ba271a1315 RC aonya polisi wanaodai rushwa kwenye baa usiku

Mon, 26 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amekemea tabia ya baadhi ya polisi wa doria za usiku kuomba hongo kwa wenye baa wanaochelewa kufunga biashara zao.

Dk Mahenge aliahidi kuzungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma kuhusu suala hilo.

Alitoa maagizo hayo jijini hapa jana baada ya kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara wa baa katika mkutano alioitisha kuwaonya wafanyabiashara kuacha kupiga muziki kwa sauti kubwa nyakati za usiku na kuchelewa kufunga biashara zao kama leseni za biashara zinavyowataka.

Wafanyabiashara hao walilalamika kwamba wamekuwa wakinyanyaswa na askari wa wanaokuwa katika magari ya polisi wakifanya doria usiku wakifdai kuwa, askari hao wanawalazimisha kutoa rushwa.

"Wafanyabiashara msikubali kutoa rushwa kwa askari hao wa doria usiku, badala yake mkubali kutoa faini lakini si rushwa au toeni taarifa kwa mkuu wa wilaya au kwa mkurugenzi wa Jiji la Dodoma," alisema Mkuu wa Mkoa Mahenge.

Mmiliki wa Baa ya Sega Makulu, Tamasha Nchimbi, alisema wamekuwa wakisumbuliwa na askari wa gari la doria wanapopitiliza hata dakika chache za kufunga, baadhi ya polisi hao wanapofika na kudai hongo.

Naye mmiliki wa Dodoma Village Resort, Eustace Bakumba, alisema polisi wamekuwa wakichukua rushwa kwenye baa usiku, vitendo ambavyo vimekuwa kero kwa wafanyabiashara hao.

Mkurugenzi wa Jiji, Joseph Mafuru alisema suala la kuongeza muda wa kufungua na kufunga baa linahitaji majadiliano zaidi, hivyo atakutana na wadau kujadili na kuwapa mrejesho.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Josephat Maganga aliwataka wafanyabiashara kuzingatia sheria za uendeshaji wa biashara kama leseni zinavyoelekeza kuhusu muda wa kufunga na upigaji wa muziki wakizingatia mahali biashara zilipo.

Ofisa Biashara wa Jiji, Donatila Vedasto aliwataka kuzingalia sheria, kanuni za leseni na kwamba, kama waliomba kuuza ‘grocery’ basi wasibadili na kuuza kama baa bila kwenda kwenye mamlaka hiyo kubadili.

Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Franklin Rwezimula, alisema wafanyabiashara wanatakiwa kufuata sheria za mazingira zinazokataza kelele na mitetemo nyakati za mchana na usiku kwa kufuata kiwango stahiki kilichopangwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz