Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC amuonya Mwita Waitara, A-Z kilichomtoa machozi

Waitara Chozi Pic Mwita Waitara

Thu, 30 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uongozi wa Serikali mkoani Mara umewaonya viongozi wa kisiasa mkoani humo kuacha kuingilia kazi ya uwekaji vigingi kwenye mpaka baina ya vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika wilaya ya Tarime.

Onyo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee wakati alipokuwa akizindua uwekaji wa vigingi hivyo, kazi inayotarajiwa kufanyika kwa muda wa siku 30.

Alisema inasikitisha kuona viongozi wa CCM, akiwamo Mbunge wa Tarime vijijini, Mwita Waitara kupinga kazi hiyo ambayo alisema inalenga kuleta suluhisho la kudumu kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya vijiji hivyo na hifadhi hiyo mgogoro uliodumu kwa zaidi miaka 40.

“Nimepigiwa simu na Waitara anasema yeye hakubaliani na shughuli hii, inasikitisha kuona kuwa kiongozi wa CCM anapingana na maamuzi yaliyotolewa na Serikali yake, maamuzi ambayo yana manufaa kwa wananchi wake,” alisema.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, hatamuonea aibu kiongozi yeyote atakayetaka kukwamisha shughuli hiyo na kuwataka viongozi hao kumheshimu, kwani anachofanya ni kutekeleza maagizo ya Serikali ambayo pia alisema kuwa hayana malengo ya kumnyanyasa mtu yeyote.

“Ukinihesimu nami nitakuheshimu, sitamuonea aibu mtu yeyote anayetaka kukwamisha kazi hii na kwa vile kinachofanyika hapa ni kwa maslahi ya wananchi anayeona hawezi kushirikiana na sisi naomba akae pembeni,” alisema Meja Jenerali Mzee.

Wakati RC huyo akizungumza hayo, jijini Dodoma, Waitara alikutana na waandishi wa habari kuzungumzia suala hilo, akisema mkuu huyo wa mkoa akiambatana na viongozi wengine wa Serikali na chama, walikwenda kwenye eneo hilo na kutoa kauli zenye utata.

Alisema kauli hizo ni pamoja kudharau shughuli za kilimo zinazofanywa na wananchi kwa muda mrefu katika eneo hilo.

Waitara alisema baada ya kauli hizo, wapinzani (hakuwataja) walikwenda katika eneo hilo na kuwaeleza wananchi kuwa yeye (Waitara) hawezi kuwasaidia na ni mchumia tumbo tu.

Alisema baada ya mkutano huo alikwenda kwa mkuu wa mkoa na kumwelezea kuwa wananchi wa eneo hilo wanahitaji ushirikishwaji kwenye utatuzi wa mgogoro huo.

Alisema kutokana na mazungumzo hayo, Mkuu wa mkoa alikubaliana na wazo la wananchi hao ambapo alimweleza hakuna vigingi vitakavyowekwa bila kuwashirikisha wahusika wa eneo hilo.

Waitara alisema baada ya kutoka kwa mkuu wa mkoa alikwenda kuitisha mkutano na kuwaeleza wananchi juu ya ahadi hiyo, lakini badala ya kutimiza ahadi yake alikwenda kuzindua vigingi katika eneo hilo la Nanungu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live