Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC akutana na watendaji kuweka mikakati ya utendaji

E7810d07b37b1763447e59b40c90a0ce RC akutana na watendaji kuweka mikakati ya utendaji

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi jana amekutana na wakuu wa wilaya na watendaji wa halmashauri zote za mkoa wa Iringa, kuweka mikakati ya namna watakavyoitekeleza Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 na maelekezo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa wakati akifungua bunge la 12.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo anataka kuona watumishi ambao ni wasimamizi na watendaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo wanakuwa na mshikamano, wanaacha kusengenyana na kudharauliana ili migongano yao iwe ni ile ya kusukuma maendeleo ya wananchi na Taifa.

“Mchakamchaka umeanza, viongozi wa mkoa, wilaya, halmashauri na wabunge na madiwani lazima kila mmoja awe na malengo ya utekelezaji wa majukumu yake kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi , maelekezo na ahadi nyinginezo… hatutaki kuona watumishi mnafanya kazi kwa majungu, fitina na chuki. Awamu hii tutaongeza ukali ili mambo yaende. Shikamaneni,” alisema Hapi wakati akifungua kikao hicho.

Akizungumzia maendeleo ya mkoa wa Iringa, Hapi alisema kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), mkoa wa Iringa unashika nafasi ya nne kuchangia Pato la Taifa (GDP) lakini bado baadhi ya watu wake wana shida mbalimbali za maisha na maendeleo.

Aliwataka watendaji kuweka mkazo katika shughuli za maendeleo ya wananchi ili kuimarisha pato la mtu mmoja mmoja na kuongeza kuwa mkoa wa Iringa una ardhi ya kutosha kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo na kama fursa hiyo ikitumika vizuri na kisasa inaweza kuwa mkombozi kwa wananchi hasa wenye kipato cha kawaida.

“Huku nyuma kulikuwa na utaratibu wa kopa ng'ombe lipa ng'ombe, angalieni namna ya kuuimarisha mpango huo. Lakini himizeni kilimo cha mazao yanayoweza kustawi vizuri na kuleta faida kwa wananchi. Mazao hayo kama ufuta na parachichi bado hayajapata mkazo wa kutosha," alisema.

Katika kutekeleza Ilani na hotuba ya Rais alisema mkoa wa Iringa utaangalia sana eneo la uwezeshaji wananchi kiuchumi na akawaagiza wataalamu wa halmashauri hizo kutumia maarifa ya kisasa kuhakikisha watu wenye shida wanapungua.

Chanzo: habarileo.co.tz