Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC akataa mashirika ya ujanja ujanja

4d12c3e5e70249e0a526f447f77560fc RC akataa mashirika ya ujanja ujanja

Mon, 19 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amesema serikali haipo tayari kufanya kazi na mashirika ya kigeni ambayo yanalenga kufanya shughuli zake za kusaidia maendeleo ya wananchi kiujanjajanja.

Kauli hiyo aliitoa wakati akipokea msaada wa bajaji tano na pikipiki tatu zenye thamani ya Sh milioni 45 kwa watu wenye mahitaji maalumu na wanaoishi katika mazingira magumu jijini Tanga uliotolewa na Taasisi ya Islamic Help .

Alisema serikali imetoa fursa za mashirika hayo kufanya kazi nchini ili kusaidiana na serikali katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi ya jamii, hivyo iwapo yamekuja kwa lengo la kufanya utapeli yatachukuliwa hatua stahiki haraka.

"Naomba niwawekea wazi serikali ya Rais Samia Suluhu inawapenda wawekezaji, ndio maana kila siku anasitiza umuhimu wa kuweka mazingira mazuri lakini shida inakuja kumekuwa na mashirika ambayo yanajisajili kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi, badala yake yanafanya utapeli hayo tutakula nayo sahani moja,"alisema.

Hata hivyo alifurahishwa na shirika hilo kwa namna ambavyo lilivyoweza kusaidiana na serikali katika ujenzi wa miradi ya maji na misaada ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Naye Mkurugenzi wa shirika hilo, Amjad Khan alisema kutoka na kufanya vizuri shughuli zake za kuwasaidia wananchi hapa nchini bajeti ya kufanya shughuli za maendeleo imeweza kuongezwa kutoka Sh milioni 500 hadi kufikia Sh bilioni 11 kila mwaka.

Alisema usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo unaofanywa na serikali umeweza kuwavutia wafadhili wa shirika hilo na hivyo kuona ipo haja ya kuongeza bajeti na kupanua wigo wa kufanya shughuli za miradi ya maendeleo ili kusaidia na serikali.

Mmoja wa wanufaika hao ambaye ni mlemavu wa viungo, Mariam Siafu alisema kwa msaada huo wa bajaji ataweza kufanya shughuli za biashara ya abiri na hivyo kuweza kujitegemea kiuchumi.

Jumla watu 18 wenye mahitaji maalumu na wanaishi katika mazingira magumu wamepatiwa msaada huo wa vyombo vya usafiri na msaada wa kibinadamu ili waweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz