Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC akanusha kuzidiwa wagonjwa wa corona

B545a08e4b913b04ffb2b519fb3ced83.jpeg RC akanusha kuzidiwa wagonjwa wa corona

Wed, 14 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Philemoni Sengati amekanusha taarifa kwa hospitali ya rufaa ya mkoa huo imeelemewa na wingi wa wagonjwa wa Covid-19.

Dk Sengati alisema taarifa hizo zilizodaiwa kusambazwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (BAVICHA) mkoani Iringa, Vitusi Nkuna ni za uongo.

Ilidaiwa kuwa Nkuna alisambaza taarifa kupitia mitandao ya kijamii kwamba Mkoa wa Shinyanga umeelemewa na wagonjwa wa Covid-19 na una uhaba wa mitungi ya oksijeni.

Dk Sengati alikanusha taarifa hizo wakati akizungumza na watumishi wa serikali na alipotembelea wagonjwa wa Covid-19 waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

“Serikali ya Mkoa wa Shinyanga tumesikitishwa na taarifa hizi ambazo zimeenezwa kwenye mitandao ya kijamii na Mwenyekiti wa Bavicha mkoani Iringa Vitus Nkuna kuwa tumelemewa na wagonjwa wa corona na hatuna mitungi ya oksijeni kitu ambacho ni uongo,” alisema Dk Sengati.

Dk Sengati alisema baada ya kusambaa kwa taarifa hizo alikwenda katika hospitali kuona hali ilivyo na akakuta hakuna wagonjwa wengi kama ilivyodaiwa.

“Mwenyekiti huyu wa Bavicha lazima serikali tumchukulie hatua kali za kisheria kwa kuzusha uongo na kuleta taharuki kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, hatukatai wagonjwa ni kweli wapo, lakini siyo wengi kama inavyoenezwa na wanaendelea kupata matibabu,” alisema.

Akiwa kituo cha mabasi mjini Shinyanga aliwataka wananchi waendelee kujikinga wasiambukizwe virusi vya corona. Aliwahimiza wanawe mikono kwa sabuni na maji tiririka, wavae barakoa, wapake vitakasa mikono na waepuke mikusanyiko.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndugile alitoa mwito kwa wananchi wanaposikia dalili za ugonjwa huo wawahi kwenda kupata tiba kwenye vituo vilivyotengwa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Kolandoto na Kituo cha Afya Kambarage.

Dk Ndugile alitaja vituo vingine kuwa ni Kituo cha Afya Tinde, Bugharama, Nyamilangano, Hospitali ya Iselamagazi wilayani Shinyanga na Hospitali ya Wilaya ya Kahama.

Alitaja dalili za Covid-19 kuwa ni kuchoka, kusikia homa, viungo kuuma, kushindwa kupumua vizuri na kuharisha.

Chanzo: www.habarileo.co.tz