Mkuu wa mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba ameongoza zoezi la ugawaji wa bidhaa zenye thamani ya Sh Milioni 12.4 zilizokamatwa wakati zikiingizwa nchini kwa njia za magendo kupitia mpaka wa Tunduma kutokea nchini Zambia.
Kindamba ameongoza zoezi hilo jana tarehe 9 Februari 2023 baada ya bidhaa hizo kukamatwa kutokana na operesheni iliyofanywa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na jeshi la polisi.
Amesema bidhaa hizo zilikuwa zinavushwa kwa njia za panya kuingia nchini huku wahusika nao wakishindwa kushindwa kuzilipia.
Amesema baada ya wenye mizigo hiyo kushindwa kulipia, wamezigawa kwa makundi maalum ikiwemo taasisi za serikali na kuongeza kuwa TRA kwa kushirikiana na jeshi la polisi, itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara wote kuhakikisha wanafuata utaratibu uliopo kuingiza bidhaa zao nchini.
Aidha, Kaimu Meneja wa TRA mkoa wa Songwe, Valerian Thadei ametaja bidhaa hizo kuwa ni sukari kilo 3,420 yenye thamani yake ni Sh. milioni 10.2, biskuti katon 96 zenye thamani yake ni milioni 1.4 na juisi aina ya apple katon 15 yenye thamani yake ni Sh,720,000 ambapo jumla ni Sh. milioni 12.4.
Taasisi zilizopata mgao huo ni shule za sekondari za Tunduma, Songwe, Vwawa, Mlangali, Simbega, Tunduma Tc, Mwl. Nyerere, Mpemba, Kafule, Chikanamilo, Maweni, Kanga pamoja na shule za msingi za na awali Tunduma na Mwenge.
Thadei ameongeza kuwa pia wamegawa bidhaa hizo katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Mbozi Misheni, Jeshi la Magereza, kituo cha Umiseta na Umitashunta ambapo tayari wahusika wamezipokea.
Aidha, amemhakikishia mkuu wa mkoa kuwa zoezi la operesheni hiyo, litaendelea ili kuhakikisha hakuna mtu anayevusha bidhaa za magendo.
Akipokea mgao huo, Mkuu wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Mbozi Misheni, Aneth Wavenza amesema atahakikisha mgao huo unatumika kulisha watoto waliopo na kwamba serikali imefanya kazi nzuri kuona umuhimu wa kugawa bidhaa hizo kwa makundi yenye uhitaji zikiwemo taasisi za serikali.
Mpaka wa Tunduma unatumika kwa nchi wanachama wa kusini mwa Afrika (SADC) na kumekuwepo na muingiliano mkubwa wa watu wanaofika kufanya biashara.