Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC aeleza undani ‘Kura Yangu Mtaji Wangu’

3b6619250267cb36b2fc2b53e0092272 RC aeleza undani ‘Kura Yangu Mtaji Wangu’

Thu, 8 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amesema ametunga kitabu kiitwacho ‘Kura Yangu Mtaji Wangu’ kuwasaidia wananchi katika chaguzi za kisiasa.

Kitabu hicho kitawapima wagombea kama wanaweza kuleta matokeo chanya ya kura wanazowapigia.

Pia kitabu hicho kinatoa nafasi kwa wapiga kura, kupima wagombea kama wanafahamu wapiga kura wanaishi mazingira gani na matamanio yao ya kimaendeleo.

Mghwira aliieleza HabariLEO kwa simu jana kuwa kitabu hicho, pia kinamwezesha mpiga kura kumpima mgombea, kama anaweza kumtumikia mpigakura kwa mafanikio.

Alisema kwa miaka mingi Watanzania wamekuwa wakipiga kura kuwachagua viongozi katika ngazi za uongozi kuanzia mitaa hadi urais.

Lakini, baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kujifanyia uwekezaji binafsi wa maendeleo, badala ya kuwekeza kwenye maendeleo ya wananchi.

“Miaka mingi wananchi wamekuwa wakiwekeza kwa baadhi ya viongozi wanaowachagua lakini hawapati matokeo, ndiyo maana katika kitabu changu nawakumbusha wananchi kwamba kura zao ndiyo mtaji wao wa maendeleo, tunapopiga kura tunamchagua kiongozi na kumpa dhamana kubwa ili tupate matokeo, tunampa matamanio yetu ya maisha katika kutumikia,”alisema.

Mghwira alisema kwa kuwa aliwahi kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa ikiwemo urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chama Cha ACT-Wazalendo, amekuwa akitafakari kuhusu mambo ya uongozi wa kuchaguliwa una maana gani hasa kwa wananchi, ndipo akaamua kuandika kitabu ili kuwapa mwanga wananchi kutambua thamani ya kura zao.

Alisema uongozi ni uwekezaji, kwa kuwa wananchi wanampatia kiongozi mtaji wa kura zao wakitarajia mambo makubwa kwa maendeleo yao, hivyo wanatakiwa kuwa makini katika kuchagua viongozi kwa sababu kupga kura ni uwekezaji muhimu kwa maisha yao.

Alisema aliwahi kuandika vitabu vingi vya kijamii, lakini hiki cha ‘Kura Yangu Mtaji Wangu’ ni cha kwanza kukiuza.

Chanzo: habarileo.co.tz