Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC aagiza wanafunzi kukimbia mchakamchaka kila asubuhi

Mchaka Mchaka Wanafunzi wa shule ya msingi wakikimbia mchakamchaka.

Fri, 22 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameagiza shule zote mkoani hapa, kuweka utaratibu wa wanafunzi kukimbia mchakamchaka ili kuwasaidia kuwa na afya, ukakamavu, uzalendo na kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Senyamule, amesema hayo jijini hapa, alipokuwa akizindua Wiki ya Wadau wa Elimu jijini hapo.

Amesema, hakuna mwanafunzi anayeweza kufanya vizuri kwenye masomo yake kama hayuko sawa kiafya, na mazoezi ndiyo njia pekee ya kuimarisha afya.

“Kupitia jukwaa hili la wadau wa elimu Mkoa wa Dodoma niagize shule zote mkoani hapa kuhakikisha zinaweka utaratibu mzuri wa wanafunzi kukimbia mchakamchaka kabla ya kuanza masomo kwa umbali fulani ili kuwafanya wanafunzi kuwa wenye afya,” amesema Senyamule.

Aidha, amesema mchakamchaka unafaida nyingi ikiwamo kuwafanya wanafunzi kuwa wenye akili na wazalendo kupitia nyimbo watakazoimba wakati wakikimbia kuwakumbusha historia ya nchi yao.

“Pamoja na faida hizo, lakini mnapokimbia mnaimba nyimbo ambazo zinawajenga wanafunzi kuwa wazalendo na kuwakumbusha historia ya taifa lenu lini hata hapo baadaye tuwe na wananchi wanalolifahamu vizuri taifa lao,” amesema.

Amesema hivi sasa kumekuwapo na idadi kubwa ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na kutofanya mazoezi.

“Mazoezi ni muhimu sana kwetu kwani hivi sasa wapo watu wengi wanasumbuliwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, lakini kama tutafanya mazoezi tunaiondolea mzigo serikali kwa kuhudumia wagonjwa.

“Naagiza shule zote mkoani Dodoma zinaweka maeneo ya kufanya mazoezi ili kutoa fursa kwa wanafunzi kufanya mazoezi yatakayosaidia kuimarisha afya zao na kuwalinda na magonjwa mbalimbali,” amesema.

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma wameunga mkono agizo hilo, wakisema kuwa ni jambo sahihi kwa kuwa mchakamchaka ni sehemu sahihi ya kuwajengea ukakamavu wanafunzi.

Chritopher Dioni, mkazi wa jijini hapa, amesema anaungana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwa hata wao wakati wakiwa wanafunzi walikuwa wanakimbia mchakamchaka ambao uliwasaidia kufanya mazoezi kabla ya kuanza masomo ya kila siku.

“Mchakamchaka unamsaidia mwanafunzi kujiweka sawa kiakili kabla ya kuingia darasani, lakini pia unaimarisha afya yake tofauti na hivi sasa ambapo shule nyingi watoto wanaletwa na gari halafu hawana muda kabisa wa kufanya mazoezi,” amesema.

Naye Sekela Kilembe amesema, wanafunzi wa miaka ya nyuma mchakamchaka uliwajenga kuwa wakakamavu na kuwafanya wazalendo kutokana na nyimbo walizokuwa wanaimba kuwakumbusha historia za nchi yao na bara la Afrika.

Awali, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Vicent Kayombo, amesema Wiki ya wadau wa elimu iliyozinduliwa jana itatumika kujadili changamoto na kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu mkoani hapa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live