Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ameagiza kukamatwa na kunyang’anywa biashara watu wanaokopesha bila kibali wala lesini kutoka Benki Kuu (BOT) ambao hukopesha fedha kwa riba kubwa maarufu mkopo umiza kutokana na biashara hizo kuwa haramu.
Akizungumza leo Jumanne Septemba 19, 2023 kwenye Kongamano la Mwalimu Spesho lililoandaliwa na benki ya NMB na kuhudhuriwa na walimu 400 kutoka Wilaya ya Geita, Shigela amesema mtu yeyote anaefanya kazi ya ukopoeshaji lazima awe na kibali na leseni kutoka BOT kinachoeleza taratibu za ukopeshaji na riba zake.
Amesema mikopo umiza inayotolewa na matajiri wa vijijini inawaumiza walimu na kusababisha washindwe kufanya kazi kwa ufanisi na kuagiza taarifa za watu hao zipelekwe kwa mkuu wa Wilaya ili aweze kuwachukulia hatua.
“Matajiri wa huko kijijini wanariba zisizoeleweka ambazo zinawafanya walimu washindwe kurejesha na kujikuta kwenye mikopo umiza na kadi zao zinashikiliwa unakopa Sh 20,000 lakini unajikuta mwisho wa mwezi una mkopo wa Sh 400,000 hizi ni biashara haramu na wakopeshaji hawana leseni kutoka benki kuu na hapa kwetu kama wapo hatutawavumilia,”amesema
Katika hatua nyingine Shigela amewataka walimu kutumia mafunzo waliyopewa yakiwemo ya namna ya kuweka akiba kabla ya matumizi pamoja na kutumia fursa zinazotolewa na benki ya NMB ikiwemo mikopo ya elimu, nyumba, vifaa vya usafiri na hata kilimo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Awali Kaimu Meneja wa benki ya NMB Kanda ya Ziwa, Dickson Richard amesema walimu wamekutanishwa ili wajadili fursa mbalimbali na kupewa elimu ya kifedha kupitia kongamano na kuwahabarisha juu ya maendeleo ya kibenki na huduma zinazowahusu.
“Mwaka jana tumezindua mpango maalum wa mwalimu Spesho na leo tumekuja kutoa elimu zaidi na kusisitiza juu ya huduma inayomwezesha mwalimu ikiwemo kutoa mikopo yenye riba nafuu, kujiendeleza kielimu yeye na watoto wake, mikopo ya biashara ndogondogo, ujenzi na vyombo vya moto pamoja na mikopo ya bima”amesema
Baadhi ya walimu walioshiriki Kongamano hilo, William Mateo na Anitha Yohana wamesema elimu waliyoipata kupitia kongamano la mwalimu Spesho litawafanya walimu kuwa na utamaduni wa kuwekeza.
Mateo amesema walimu wengi hawana utamaduni wa kuweka akiba na hiyo ndio moja ya sababu ya walimu kuingia kwenye mikopo kausha damu ambayo mbali na kusababisha mwalimu akose mshahara lakini inawafanya pia wawe watoro shuleni wakiogopa kukamatwa na waliowakopesha.
“Hapa tumeelekezwa namna ya kuweka akiba na namna ya kutunza kwa ajili ya watoto kuna mambo mengi tumejifunza mbayo mwisho wa siku yatatuwezesha kupanga vizuri fedha tunazopata”amesema