Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC aagiza vitambulisho vya ‘wamachinga’ virudishwe

2a023fb3c029abdc286e01f284122867 RC aagiza vitambulisho vya ‘wamachinga’ virudishwe

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mwanza, John Mongella, amezipa siku tatu halmashauri zote mkoani Mwanza kurejesha vitambulisho vya wajasiriamali vilivyobaki baada ya vingine kuuzwa kabla ya kuanza kusambazwa vipya.

Mongella alitoa agizo hilo jana katika Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Mwanza (RCC) kilichofanyika jijini hapa.

Alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa, Emmanuel Tutuba, kutoa muda huo wa siku tatu katika kutekeleza agizo.

“Hao wape muda wa hadi Jumatatu kurejesha vitambulisho hivyo kwani tumeshawakumbusha muda mrefu mno, lakini hawatekelezi mwito huo,” alisema.

Awali, Tutuba alisema mwaka jana vitambulisho 88,000 vilitolewa kwa ajili ya kusambazwa kwa walengwa, lakini vitambulisho 65,912 ndivyo vilinunuliwa kwa Sh bilioni 1.3.

Tutuba alisema vitambulisho vilivyonunuliwa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) vilifikia zaidi ya asilimia 74.9 ya lengo lake.

“Hata hivyo cha kushangaza mpaka sasa kwa vile vitambulisho vilivyobaki havijarudishwa licha ya halmashauri hizo kutakiwa kufanya hivyo mara kwa mara,” alisema.

Kwa mujibu wa katibu tawala wa mkoa huyo, hadi sasa vitambulisho vya 15,299 vimerejeshwa huku vingine 6,789 vikiwa havijarejeshwa katika Ofisi ya Mkoa wa Mwanza.

Tutuba alitaja halmashauri ambazo hazijarejesha na idadi ya vitambulisho katika mabano kuwa ni Ilemela (1108), Kwimba (169), Magu (291), Jiji la Mwanza (2,836), Buchosa (2,026), Sengerema (797) na Ukerewe (62).

Chanzo: habarileo.co.tz