Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC aagiza utengenezaji mipango miji haraka

Omary MKUU wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba,

Wed, 22 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri wakishirikiana na watumishi wa ardhi, kutengeneza mipango miji haraka yenye kuzingatia uhifadhi mazingira, maeneo wazi ya watoto na kutenga maeneo ya viwanda vidogo vidogo vinavyoongeza thamani ya mazao mbalimbali yanayozalishwa kwa wingi.

Mgumba alitoa kauli hiyo juzi akizungumza na wakuu wa Idara ya Ardhi na watumishi wengine wa mkoa huo.

Alisema Mkoa wa Songwe bado haujapangwa vizuri hali inayosababisha wananchi kutozingatia uhifadhi wa misitu, maeneo ya wazi kwa ajili ya watoto kucheza, kuvamia na kujenga maeneo yenye rutuba yanayofaa kwa kilimo.

Alisema watumishi wa ardhi mkoa wakishirikiana na wakurugenzi wanatakiwa kuanza mara moja kurasimisha ardhi na kupanga miji kulingana na uhitaji wa halmashauri huku uhifadhi wa mazingira ukifuatwa ili miji iendelee kuwa ya kijani.

"Maeneo yarasimishwe na kupangwa kulingana na uhitaji wa viwanda, biashara na kilimo na ufugaji. Kuna maeneo ni mazuri kwa kilimo, lakini yamevamiwa na kuwa makazi ya watu," alisema Mgumba.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Songwe, Suma Mwakasitu, alisema mpaka sasa ni Halmashauri ya Mji Tunduma pekee ambayo tayari imepima na kupangilia mji wake.

Alisema pamoja na mkoa kuwa mpya wamejipanga kuhakikisha halmashauri zote za mkoa wa Songwe kupima na kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo, viwanda, biashara utunzaji uhifadhi wa misitu na makazi.

"Tuna mpango kabambe kuhakikisha Mkoa wa Songwe kuwa kwenye mpangilio mzuri tukishirikiana na wakurugenzi wa halmashauri zote," alisema Mwakasitu.

Kwa upande wake, mkazi wa Vwawa, Sophia Mwashiuya, alisema kukosekana kwa mipango miji hususan katika mji wa Vwawa husababisha wananchi kushindwa kusaidiwa wanapopata majanga kama ya moto.

Alisema siku hizi watoto hawana maeneo ya michezo wanapokuwa nyumbani, jambo ambalo huchangia kupoteza vipaji vyao vya michezo kama riadha na mpira wa miguu.

Chanzo: ippmedia.com