Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imeshatoa tahadhari ya uwepo wa mvua kubwa, Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda, amewataka TANROADS na TARURA mkoani humo kuhakikisha mitaro yote inayotumika kutiririsha maji itolewe uchafu ili maji yakianza kupita yasiwe na kizuizi.
Ameyasema haya mara baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi na kuwataka wakuu wa wilaya zote mkoani Simiyu kuhakikisha suala la usafi linakuwa endelevu kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.
Katika hatua nyingine Dkt. Nawanda amesema ni marufuku mtu yoyote kutupa taka ovyo na atakayebanika faini yake ni shilingi elfu hamsini ambazo zitaingia serikalini na kutumika kwenye shughuli za usafi wa mazingira huku akisisitiza kuwa endapo mwananchi atasaidia kumtaja mtupa taka ovyo atapewa shilingi elfu kumi kati ya ile faini.