Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC aagiza Mkuu wa Shule ahamishwe matokeo kidato 4

Fc7e4579fec261b4a458dcd3c818af64 RC aagiza Mkuu wa Shule ahamishwe matokeo kidato 4

Fri, 16 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa (RC) wa Geita, Robert Gabriel amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa kumhamisha Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Butobela iliyopo Kata ya Butobela wilayani Geita baada ya shule hiyo kushika nafasi ya mwisho kimkoa kwa kwa miaka miwili mfululizo katika matokeo ya kidato cha nne.

“Yaani shule inakuwa ya mwisho mara mbili, hii si sawa; Kaimu Katibu Tawala lete mkuu wa shule mwingine hapa, ndani ya siku tatu awe amepatikana,” aliagiza.

Alitoa agizo hilo wiki hii alipotembelea shule hiyo katika mwendelezo wa ziara yake kukagua utekelezwaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kusisitiza agizo hilo kutekelezwa haraka akidai mkuu huyo ameshindwa kumudu majukumu yake.

Alieleza kutofurahishwa na mwenendo wa kitaaluma katika shule hiyo iliyoshika nafasi ya mwisho kimkoa kwa matokeo ya Mtihani wa Taifa kwa Kidato cha Nne Mwaka 2019/2020 na 2020/2021.

Alimtaka mdhibiti ubora wa shule katika mkoa huo, kumpatia taarifa ya kina ya sababu ya matokeo hayo mabaya shuleni hapo.

Akizungumza kwa simu kuhusu hatua iliyochukuliwa, Mkuu wa Shule hiyo, Michael Mwendwa ambaye wakati huo alikuwa safarini, alisema changamoto kubwa zilizopo ni shule kukosa huduma rafiki kama maji, umeme, walimu wa sayansi na wanafunzi wengi wanaishi mbali na shule kutokana na kukosa mabweni.

Alisema mara kadhaa amefanya mkakati wa kuleta maendeleo ya kitaaluma, ikiwemo kupika chakula cha mchana pamoja na kuratibu michango ya kulipa walimu kwa muda wa ziada, lakini haukuungwa mkono.

Alisema na hata barua za kuelezea changamoto za shule hazijibiwi, ikiwemo ya mwisho aliyoiandika Februari Mosi mwaka huu kwenda kwa Mratibu Elimu Kata, Mkurugenzi Mtendaji na Katibu Tawala mkoa.

“Nimehamia shule hiyo tangu mwaka 2018, nimekuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Busanda nimekaa miaka saba haikuwahi kuwa ya mwisho, nimekaa Chigunga miaka mitano haikuwa ya mwisho kwa vile hakuna changamoto kubwa kama hapo,” alisema.

Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Alipipi Mwakihaba, alisema pamoja na utetezi wa mkuu huyo wa shule, alishawahi kuitwa na kuonywa zaidi ya mara tatu kutokana na mwenendo mbaya wa kitaaluma shuleni hapo, lakini hakuna mabadiliko yaliyoonekana.

Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Donald Nsoko, alisema utetezi wa mkuu wa shule huyo kuhusu wanafunzi kutopata chakula cha mchana ni dhaifu kwani kuna shule nyingi ambazo hazitoi chakula cha mchana lakini, zinafanya vizuri kitaaluma.

Alisema mkuu wa shule huyo amekuwa mzembe kufika kwenye kituo chake cha kazi kwa wakati kisingizio cha kukaa Mji Mdogo wa Katoro huku akiwa hana sababu za msingi japo ni hali iliyosababisha usimamizi hafifu wa shule

Chanzo: www.habarileo.co.tz