Mkuu wa mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amefafanua kuwa sababu za kuwasimamisha kazi Mganga mkuu wa halmashauri ya mji Korogwe, Salma Swedi na Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Korogwe, Magunga Dkt. Heri Kihwale ni kutokana na kuchelewa kufika hospitalini kuwahudumia majeruhi
Akizungumza katika kipindi cha Supa Breakfast kinachorushwa na EARADIO Mgumba amesema, si kwamba watumishi hao walichelewa kufika eneo la ajali kama ilivyosemekana hapo awali.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 4 na nusu usiku wa Februari tatu mwaka huu ambapo watumishi hao walifika hospitalini saa kumi kasorobo alfajiri ya Februari nne.
"Ajali ile ilitokea saa nne na nusu usiku na madaktari wamefika kwenye kituo chao cha kazi saa 11 kasoro robo asubuhi wakati majeruhi wa kwanza amefikishwa saa tano, ni uzembe wa madaktari.
"Daktari wa zamu alipopokea tu majeruhi wa kwanza na miili aliwapigia simu wote, Mkuu wa wilaya ametoka kilomita 70 kafika saa saba usiku akawapigia simu tena wakamwambia wamepokea taarifa na wametoa maelekezo, anayesema hivyo amelala kwenye nyumba anakoshi kwenye eneo la hospitali.
"Haiingii akilini anayeishi kilomita 70 afike kabla ya anayeishi mita tano, haiingii akilini akilini kwamba RTO na viongozi wengine wa mkoa wanaoishi Korogwe wawahi kufika hospitalini kabla ya daktari mwenyeji," amesema Omary Mgumba, Mkuu wa mkoa wa Tanga.