Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Tabora awafunda wakuu wa shule

60b4bc9db848c91254834f9a9b3b3b1b.jpeg RC Tabora awafunda wakuu wa shule

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati amewataka walimu wakuu waepuke kujenga makundi miongoni mwa walimu wanaowaongoza.

Alisema hayo mjini Tabora jana wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania (TAPSHA).

Ukutano huo ulikuwa ukijadili mambo mbalimbali ikiwamo mapambano dhidi ya mimba kwa wanafunzi, utoro, rushwa katika mitihani na mbinu za kuongeza ufaulu katika mitihani ya kitaifa.

“Kusipokuwa na makundi walimu wote watajiona kitu kimoja na kufanya kazi kwa bidii,” alisema.

Dk Sengati alisema hatua hiyo pia itasaidia kuwa na ushirikiano ambao utaongeza juhudi katika ufundishaji wanafunzi na kuuwezesha mkoa kuongoza katika mitihani ya kitaifa.

“Walimu wakuu ni lazima wahakikishe wanaweka mazingira mazuri na kuwaongoza vizuri walimu walio chini yao ili waweze kufanya kazi kwa bidii na moyo wa uzalendo katika kufundisha kwa ajili ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuuwezesha mkoa wa Tabora kuwa sehemu ya maeneo mengine nchini kuja kujifunza mbinu bora za ufundishaji.”

"Hatutasita kuwachukulia hatua walimu wakuu ambao wanawagawa walimu na kusababisha shule zao kuwa na ufaulu hafifu na kuufanya mkoa kushika namba za chini. Walimu wakuu wanatakiwa kuwa mfano mzuri wa uongozi kwa walio chini yao, wale watakaoshindwa kuongoza wenzao kwa misingi ya umoja na mshikamano tutawaondoa katika nafasi zao na kuwapa ambao watatusaidia kuufanya mkoa wetu uwe darasa la wengine kujifunza," alisema.

Aidha, Dk Sengati aliwataka walimu wakuu kuendelea kuwachukulia hatua kali walimu wasio waadilifu na wenye tabia mbaya za kujihusisha kimapenzi na wanafunzi na hivyo kuwasababishia kurudi nyuma kitaaluma na wengine kukatisha masomo kwa ujauzito.

Aliwaagiza walimu wakuu kuendelea kusimamia ujenzi wa miundombinu ya shule kwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za umma.

Alisema walimu wakuu wanatakiwa kuendelea kuchukua hatua kwa wazazi wa wanafunzi watoro kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili kutoa fundisho kwa wazazi wengine.

Awali Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia elimu mkoa wa Tabora, Michael Ligola aliwataka walimu wakuu kuwa na vipindi katika madarasa yanayokuwa na mitihani ya kitaifa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za walimu wanaofundisha madarasa hayo

Chanzo: habarileo.co.tz