MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amewataka watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wafanyabiashara mkoani humo, kutojenga mazingira ya chuki wakati wa ukusanyaji kodi.
Alitoa jana rai hiyo wakati wa kikao cha wadau wa kodi, ambao alisema kuwa iwapo pande zote mbili zitafanya kazi kwa uwazi bila ya kificho, hakuna umuhimu wa uwepo wa uhasama wala chuki baina yao.
Alisema kuwa kodi ndio uti wa mgongo wa taifa lolote, kwa hiyo ni lazima kujipanga vizuri kuhakikisha kwamba watumishi TRA na wafanyabiashara hawajengeani mazingira ya chuki, kwa kudhani kwamba wafanyabiashara ndio wanakwepa kodi au watu wa TRA wanakuja na makadirio yasiyokuwa na utaratibu.
Alitaka watumishi kufanya kazi kwa kufuata kanuni za utumishi wa umma zinavyoelekeza na wafanyabiashara wafanye shughuli zao kwa utaratibu mzuri.
“Hakuna sababu ya kuibiana wakati mifumo ya ukusanyaji imetengenezwa na inafanya kazi kwa utaratibu, hivyo tunaweza kukusanya kodi kwa ufanisi na kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Specioza Owure alisema bado wanaendelea kutoa elimu ya kodi na umuhimu wa wafanyabiashara kutoa risiti wakati wa kuuza bidhaa kwa mteja.
Alitaja changamoto kubwa ilipo ni bado wananchi wengi hawana utaratibu wa kudai risiti wanapofanya manunuzi. Alisema kudai risiti ni haki yao.
“Wananchi wajenge tabia ya kudai risiti kwani hiyo inaonyesha uzalendo kwa nchi yao. Unapodai risti nawe unakuwa sehemu ya walipa kodi, naomba wafanyabiashara kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiyari,” alisema.