Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amewaagiza waratibu wa UKIMWI nchini kuzungumza na jamii kwa uwazi kuhusu mabadiliko ya tabia katika kujikinga na maambukizi ya VVU ifikapo 2030 kuwe na Tanzania isiyokuwa na UKIMWI.
Akizungumza jana Februari 20,2023 wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa taarifa ya mapitio ya fedha za UKIMWI kwenye sekta za umma na sekta binafsi ya mwaka 2022 iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana aalisema iwapo jamii itaelewa vizuri na ikakubali kubadili tabia Tanzania itafikia malengo ya Dunia ya 2030 ya kumaliza UKIMWI.
Serukamba alisema kuwa Serikali imekua ikipambana kudhibiti maambukizi ya VVU pamoja na madhara yake kwa zaidi ya miaka thelathini, ambapo kwa kiasi kikubwa mapambano haya yanategemea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za UKIMWi,ambapo amefafanua kuwa kwa mahitaji kwa mwaka ni takribani Sh. Trilini 1.3.
Aidha, aliongeza kuwa utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI umekua ukipata fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali hivyo ni muhimu kufanya mapitio ya fedha zinazotumika kwenye afua hizo ili kubaini mchango wa taasisi za sekta ya umma na mchango wa taasisi za sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kutambua Maeneo ambayo mchango huo unapelekwa kulingana na afua za VVU na UKIMWI lakini muhimu zaidi kutambua upungufu uliopo wa fedha katika kutekeleza afua za VVU na UKIMWI hapa ili Kuhakikisha utekelezaji wenye tija kwa Taifa, Jamii na mtu mmoja mmoja.
Akifafanua umuhimu wa kufanyika kwa zoezi la Mapitio ya Fedha za UKIMWI kwenye Sekta ya Umma na Binafsi (Public and Private Expenditure Review) ni kuwa zinaisaidia serikali kufahamu kiwango cha matumizi ya fedha za UKIMWI kinachopangwa na Sekta ya Umma na Binafsi.
Pia kufahamu maeneo ambayo fedha hizo zinaelekezwa, kujua kiwango cha utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI ili kubaini mchango wa sekta ya umma na binafsi katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Aidha, mapitio ya fedha za UKIMWI husaidia kubaini changamoto katika utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI nchini na kuweka mikakati ya kuzitatua.
Serukamba ameyataja mafanikio ya mafanikio yaliyotakana na zoezi hilo kuwa ni pamoja na kuboresha ugawaji wa rasilimali fedha za UKIMWI kulingana na afua zinazotekelezwa hapa nchini, kuimarisha mikakati ya kuhamasisha sekta binafsi na sekta za umma kupanga na kutekeleza shughuli za VVU na UKIMWI kwenye maeneo yao pamoja na kukuza mchango wa sekta ya umma na sekta binafsi katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI hapa nchini.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TACAIDS, Yasini Abasi alisema kuwa uhitaji wa fedha za UKIMWI bado ni mkubwa kwani kwa sasa wafadhili wanaendelea kupungua na hivyo kuitaka jamii kuendelea kuchangia mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI ili hata pale itakapo tokea waansitisha basi Mfuko uwe na fedha za kutosha kwa ajili ya huduma za UKIMWI.
Kikao hicho kiliwashirikisha waratibu wa UKIMWI kutoka baadhi ya Wizarani, Halmashauri na Mikoa.