Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema hataki kusikia wakuu wa wilaya zilizopo katika Mkoa wake wakiwaweka ndani watumishi wa umma.
Mtaka ametoa kauli hiyo jana Ijumaa Agosti 17, 2018 wakati akifunga kikao cha madaktari wa mikoa na wilaya zote nchi nzima uliofanyika mjini Dodoma.
“Sisi viongozi tuwalinde watumishi wetu, mimi nilipoenda kuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu niliwaambia wakuu wangu wa wilaya kuwa sitaki kusikia mtumishi wa umma kuwekwa mahabusu,” amesema Mtaka.
“Wakati mwingine ukiona matamko ya wanasiasa kwenye maeneo ya kazi unajiuliza hivi RM0 (mganga mkuu wa mkoa) anakaa kwenye kikao kushauri haya yatokee? Kwenye mkoa wangu hutaona huu upuuzi.”
Agosti 14, 2018 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alikemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo kuwaweka watu ndani.
Aliwataka wakuu hao kuhakikisha wanasoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ili kufanya kazi kwa weledi.
Katika siku za hivi karibuni, wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia ‘sheria ya saa 48’ kutoa adhabu kwa kuwaweka baadhi ya watu mahabusu.
Mamlaka hiyo wamepewa kupitia Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 na hutakiwa kutumia amri ya kumweka ndani-kwa muda usiozidi saa 48-mtu au kundi la watu ambao kubaki kwao nje kunaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii.
Baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakitumia sheria hiyo kama adhabu au hukumu, badala ya malengo yaliyowekwa ya kulinda usalama wa watu wengine.