Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Simiyu atilia shaka matumizi ya bilioni 754

Simiyu Bnm RC Simiyu atilia shaka matumizi ya bilioni 754

Tue, 20 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda, ameukataa mradi wa bwawa la maji katika Kijiji cha Zebeya Wilaya ya Maswa humo lililofanyiwa ukarabati kwa gharama ya Sh Milioni 754 akitilia shaka matumizi ya fedha hizo ikilinganishwa na kazi iliyofanyika

RC Nawanda, amefika na kujionea ukarabati wa Bwawa hilo na kudai fedha zilizotumika hazilingani na kazi iliyofanyika

"Mimi nimekuja kuona huu mradi wenu. Mimi nimekuja hapa bila kumuonea mtu. Mimi mwenzenu naungana na wananchi wenzangu mimi sijaridhishwa na huu mradi hata kidogo kwa hizo fedha Milioni 754, zilizotumika hapa (kukarabati) mimi sijaridhika nazo," amesema RC Nawanda. 

Mapema wakizungumzia ukarabati wa Bwawa hilo, mmoja wa wa wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Zebeya, diwani pamoja na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo, wamesema mradi huo unastahili kuhojiwa juu ya matumizi ya Sh Milioni 754, hali iliyoungwa mkono na mkuu wa mkoa huo

"Kwa jinsi lambo (bwawa) lilivyochimbwa kiasi hiki, mimi siku ya kuja kukabidhi (kukabidhiwa mradi kwa Serikali ya kijiji) baba (mkuu wa mkoa) mimi sijahusishwa, sijashirikishwa. Hata taarifa sikupewa," amesema Diwani Sadick.

"Sisi kama Serikali ya Kijiji (Cha Zebeya) Mhe mkuu wa mkoa, sisi kwa kweli hatujaridhika jinsi ya uchimbaji.

Lakini tulihoji, tulihoji ikafika sehemu nyingine wanaonekana wabaya (viongozi wa kijiji) wakati wanahoji," amesema Ndakama Mjumbe wa Serikali ya Kijiji.

"Mhe mkuu wa mkoa hebu hili suala liangaliwe kwa kina. Na kama kuna wizi umeonekana, watu wameweza kuufanya mradi huu kuwa chanzo cha fedha zao mfukoni, basi hatua zinazostahili zichukuliwe kwa sababu hizi fedha ni za Watanzania," amesema Mbunge Nyongo.

"Kwa mantiki hiyo basi leo nataka niunde timu hapa. Injinia wangu wa mkoa, injinia wangu wa RUWASA, injinia wa wilaya na wataalamu wengine ambao nitawaongeza, nawapa wiki tatu siku 21 kwa kushirikiana na watu wa bonde (Maafisa wa Bonde la Ziwa Victoria) waje wakae, waipitie BOQ, wapitie taarifa zao zote halafu tarehe 15 mwezi wa kwanza waniretee hiyo ripoti," amesema RC Nawanda.

Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dk. George Lugomela, alikabidhi mradi huo akisema umekamilika pasipo na mawaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live