Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Shigela ataka mafundi wenye leseni wawezeshwe kukagua umeme

UMEME Vunjwa RC Shigela ataka mafundi wenye leseni wawezeshwe kukagua umeme

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: mwanachidigital

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ameshauri kuwawezesha mafundi wa umeme wa mtaani wenye leseni za Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (Ewura), kukagua mifumo ya umeme ili iwe rahisi Shirika la Umeme (Tanesco) kupeleka nishati kwenye majengo ya umma.

Shigella amesema utaratibu uliopo sasa ili jengo la umma liunganishiwe umeme ni lazima likaguliwe na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa). Lakini na kutokana na uchache wa nguvu kazi na wingi wa majengo yanayohitaji nishati hiyo kumekuwa na ucheleweshwaji unaokwamisha wananchi kupata huduma kwa wakati.

Akizungumza leo Februari 29, 2024 kwenye semina ya kuwajengea uwezo wadau wa Ewura iliyohusisha watumishi wa Tanesco na Temesa, mafundi wa umeme na wanafunzi kutoka vyuo vya ufundi, Shigela amesema yapo majengo yaliyokamilika yaliyojengwa kwa zaidi ya miaka miwili na hadi sasa hayana umeme kwa kuwa Temesa hawajafika kukagua.

“Ni vema tukafanya reforms (mageuzi) kwenye mifumo ili huduma zifike mapema kuna zahanati zimejengwa huko vijijini zina miaka miwili hazifanyi kazi, ukiuliza unaambiwa Tanesco hawajaleta umeme, ukiwahoji Tanesco wanasema Temesa hawajafanya ukaguzi.

“Kwa nini hawa mafundi wanaopewa leseni na Ewura wasikague?” amehoji Shigella.

Akizungumzia ushauri huo, Meneja wa Temesa mkoani Geita, Mahangaiko Nguruma amesema tatizo lipo kwenye miradi ya halmashauri ambayo wanatumia mafundi wa mtaani wasio na leseni na wakati wa ukaguzi inabainika changamoto ambazo haziruhusu wao kutoa kibali kwa Tanesco.

“Kuna changamoto kubwa kwa mafundi unaweza kukuta nyumba ya mtumishi ina vyumba viwili lakini vifaa vya umeme vilivyotumika ni vile vinavyotumika kwenye umeme wa viwandani.

“Hii inaongeza gharama kwa Serikali na pia ni hatari mimi niwashauri watu wa halmashauri ni vema wakati wananunua vifaa wawasiliane na Temesa washauriwe na wataalamu kabla ya kununua,” amesema Nguruma.

Hata hivyo, amesema endapo wenye leseni wakikaguliwa na kazi zao zikiwa nzuri watawasiliana na Temesa makao makuu kuona namna ya kuwapa kibali kwenye majengo yenye vyumba vichache, ili kufanya kazi kama alivyoshauri na Shigela.

Naye David Josia mwenyekiti wa mafundi umeme Mkoa wa Geita, amesema wanashindwa kufanya kazi licha ya kuwa na leseni za Ewura kwa kuwa Tanesco wanazikataa, huku wakitakiwa kupita Temesa kupata kibali jambo ambalo halipo kwenye sheria za Ewura.

Kuhusu uwekwaji wa vifaa visivyo na ubora na vile visivyo na sifa kwenye jengo husika, amesema changamoto nyingine ni watumishi wa halmashauri kuwachukua mafundi vishoka wasio na leseni ili wapate asilimia 10.

Meneja wa Ewura Kanda ya Ziwa, George Mhina amesema kanda hiyo ina mafundi wenye leseni 1,108.

“Ushauri uliotolea na mkuu wa mkoa tutaufanyia kazi kwani utasaidia kufikisha huduma mapema,”amesema.

Pia amewatahadharisha wananchi kuacha kutumia mafundi umeme wasio na leseni, kwa kuwa ni hatari na inaweza kusababisha madhara kwenye nyumba zao.

Chanzo: mwanachidigital