Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Sendiga aamuru mifugo 800 iliyokamatwa Hifadhi ya Tarangire iachiwe

Sendiga Web RC Sendiga aamuru mifugo 800 iliyokamatwa Hifadhi ya Tarangire iachiwe

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amehitimisha mgogoro uliokuwepo kati ya wafugaji wa Kijiji cha Kimotorok kilichopo Wilaya ya Simanjiro na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa kuachia mifugo zaidi ya 800 iliyokuwa inashikiliwa.

Mifugo hiyo – ng’ombe, mbuzi na kondoo ilikuwa inashikiliwa na uongozi wa Hifadhi ya Tarangire ukidai wafugaji hao waliingiza kwenye eneo la hifadhi.

Akizungumza leo Januari 17, 2024 baada ya kurejesha mifugo hiyo kwa wafugaji, Sendiga amewaagiza viongozi wa kata na vijiji kusimamia makubaliano na maelekezo ambayo yanapitishwa na Serikali.

“Kila vikao vikifanyika mnapaswa kuwaambia wananchi ukweli pasipo kuwaficha ili wapate uelewa juu ya uamuzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa ili kuepusha migogoro isiyo na tija,” amesema Sendiga.

Amewataka wananchi hao waendelee kutii sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na pia wahifadhi nao wajielekeze zaidi katika utoaji wa elimu na kuboresha uhusiano kati yao na wafugaji.

Hata hivyo, mkuu wa mkoa ameuelekeza toa uongozi wa Hifadhi ya Tarangire kuwaacha wafugaji waendelee kupata huduma za mifugo yao ambazo bado zinapatikana hifadhini humo, kama vile sehemu za kunyweshea mifugo.

Uamuzi huo umepokewa kwa furaha na wafugaji hao na diwani wa Kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Mardadi) amemshukuru mkuu wa mkoa kwa kufanikisha jambo hilo.

Lesenga amesema mbali na mifugo, wafugaji sita wa Kijiji cha Kimotorok nao walikamatwa na ng'ombe 160, mbuzi 260 na kondoo 340.

Amesema askari wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire wamekamata mifugo hiyo ilhali haikuwa inachungiwa ndani ya hifadhi hiyo.

Mkazi wa Kata ya Loiborsiret, Dk Frank Oleleshwa amesema mgogoro wa mara kwa mara dhidi ya hifadhi hizo na wananchi ilikaribia kupata mwafaka wa kudumu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda kamati ya mawaziri wanane wa kisekta.

Oleleshwa amesema kamati ya mawaziri hao ambao walifika hadi Kimotorok ilishamaliza kazi yake, kinachosubiriwa ni utekelezaji wa mapendekezo lakini wanaona kimya.

“Nachoweza kushauri kwa sasa walio karibu na mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka wamshauri amuulize Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, swali la moja kwa moja bungeni, kwa nini taarifa ya kamati hiyo haijawekwa hadharani kwa umma na kwa nini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi leo?” amesema.

Mmoja kati ya wafugaji ambao mifugo yao ilikamatwa, Peter Loishiye ameiomba Serikali kuhakikisha mgogoro wao na hifadhi unamalizika kwa kuwa wafugaji wanaonewa kila mara na mifugo yao kukamatwa kimakosa.

“Ifike mahali uonevu huu uishe kwani ni muda mrefu sasa tuna mgogoro kati yetu na Tarangire na Mkungunero, ambao wanakamata mifugo yetu na kusababisha migogoro, jambo ambalo halina tija kwetu,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live