Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Sanare awaonya wabunge, kuwachongea kwa wapiga kura wao

89377 Sanare+pic RC Sanare awaonya wabunge, kuwachongea kwa wapiga kura wao

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (RC) nchini Tanzania, Loata Ole Sanare amekasirishwa na baadhi ya wabunge wa mko huo wasioshiriki vikao na shughuli mbalimbali za kiserikali bila kutoa taarifa na kuwataka kubadilika la sivyo atafikisha ujumbe kwa wananchi waliowachagua.

Amesema pamoja na wabunge hao kupelekewa barua ama ujumbe wa kuhudhuria vikao bado wameonekana kukaidi na kibaya zaidi wamekuwa hawatoi udhulu huku akihoji wanapokwenda bungeni wanachangia ama kutetea nini kuhusu wananchi wao.

Mkuu huyo wa mkoa amesema hayo leo Ijumaa Desemba 20, 2019 kwa nyakati tofauti katika kikao cha Bodi ya Barabara na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).

Ole sanare amesema kuitwa kwa wabunge katika vikao hivyo ni muhimu kwa ajili ya maandalizi ya bajeti ya mkoa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini wabunge hao wameshindwa kuhudhuria vikao hivyo na kutoa michango yao muhimu jambo ambalo linawanyima fursa wananchi kuwaletea maendeleo yao.

“Hivi ni vikao muhimu kwetu sote na wabunge kama wawakilishi wa wananchi wanapaswa kuwepo ili wanapokwenda bungeni wajue wanaenda kuwatetea nini wananchi wao, sasa kama hawapo hapa wakifika huko wanatetea nini,” amesema.

“Hivi ikitokea katika bajeti ijayo wakakosa fedha za miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao watalaumu kweli,” amehoji Sanare

Amesema mkoa una idadi ya wabunge 14 lakini walioudhuria vikao hivyo ni wanne na kwamba wengi 10 hawakuonekana na wala hajapokea taarifa ya udhuru wao.

 

Amesema katika kikao cha kujadili maendeleo ya elimu hali ilikuwa hivyo hivyo huku wakitambua suala hilo linawagusa watoto wa wapiga kura wao kwakuwa mkoa umefaulisha watoto wote ambao wanapaswa kuanza masomo ya kidato cha kwanza Januari 2020.

Ole Sanare amesema hata alipokuwa akifanya ziara ya kujitambulisha katika wilaya baadhi ya wabunge hawakuonekana na badala yake alikutana na wananchi pamoja na watendaji wa Serikali katika maeneo hayo.

Amesema yapo baadhi ya maeneo mengine wananchi wanalia na kulalamika kutowaona wabunge kwa muda mrefu, hivyo kushindwa kuwasilisha kero zao jambo ambalo linawakatisha tama wananchi.

Katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro (RAS), Emanuel Kalobelo amesema vikao hivyo vilisogezwa mbele ili kutoa fursa kwa wabunge hao kuweza kushiriki vikao hivyo kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya mkoa kutokana na baadhi walipojulishwa wameeleza katika vikao vya kamati zao bungeni lakini kwa kipindi hiki hakuna.

Wabunge walioweza kuudhulia vikao hivyo ni Dk Haji Mponda (Malinyi-CCM), Prosper Mbena (Morogoro Kusini-CCM), Dk Christina Ishengoma na Dk Jasmine Tiisekwa wote wa viti maalum kutoka CCM.

Wabunge ambao hawakuhudhuria ni; Susan Kiwanga (Mlimba), Peter Lijualikali (Kilombelo), Devota Minja (Viti Maalum) na Joseph Haule maarufu ‘Profesa J’ (Mikumi) wote hawa ni wa Chadema.

Chanzo: mwananchi.co.tz