Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Ruvuma ataja mkakati kumaliza udumavu kwa watoto

Ruvumaaaaaa Ruvumaaaa.png RC Ruvuma ataja mkakati kumaliza udumavu kwa watoto

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma (RC), Kanali Laban Thomas ameagiza kila familia mkoani humo ihakikishe inapanda mti mmoja wa matunda na kuanzisha bustani za mbogamboga kwenye kaya na au nyumba ya kupanga ili kutatua tatizo la udumavu.

Pia, amewataka wananchi kuwekeza nguvu zao kwenye upandaji miti kama walivyowekeza kwenye mazao mengine.

RC huyo alitoa maagizo hayo juzi Jumamosi, Januari 6, 2024 wakati wa uzinduzi wa upandaji miti kimkoa uliofanyika kwenye shamba ya Gereza la Kitai wilayani Mbinga.

Amesema ni ukweli usiopingika licha ya mkoa wa Ruvuma kuongoza kwa uzalishaji wa chakula lakini bado unakabiliwa na tatizo la udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano.

Kutokana na hilo, amesema ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa kwa kushirikiana na Serikali ambapo ameagiza kila kaya kupanda miti ya matunda na kuitunza.

"Naagiza kila familia ipande miti ya matunda na kuitunza miti iliyopandwa na ambayo wanaipanda leo, wapande miti kwenye vyanzo vya maji, kwenye barabara maeneo ya taasisi zote na kuitunza ikiwa ni pamoja na kuanzisha bustani za mboga mboga ili kuondoa udumavukwa watoto.

"January 19 Nitaanzisha kampeni maalum ambayo kila mwezi tutakuwa tunapanda miti ya matunda mipapai, miparachichi, lengo kuwabadilisha watu wetu kwani wanafanya kazi sana wapande ili matunda yasaidie katika tatizo la udumavu,"

"Pia upandaji miti ya kibiashara, ufanyike kuwa kilimo cha biashara kwani watu wengi wanatajirika kutokana na kilimo cha miti. Mfano mche mmoja wa kahawa ukiutunza vizuri unapata kilo tano mbichi na ukikausha unapata kilo moja ambayo inakuletea Sh4000.Ekari moja ya shamba la kahawa inakupandwa miche 1200 ukizidisha unapata Sh4,000,000 hii ni pesa nyingi," amesema RC Laban.

Amesema, miti ina faida kubwa kwani ukisimamia vizuri inaleta utajiri na mwaka kesho apatiwe taaarifa ni miti mingapi imeota na mingapi imekufa.

Mhifadhi mkuu TFS Mbinga, Kelvin Mpiluka alisema miche iliyooteshwa Mbinga kutoka taasisi na vikundi mbali mbali ni miti ya mbao 2,156,992,vyanzo vya maji miti iliyopandwa 54,968,matunda 173,585 mapambo na kivuli 6,942.

Mkuu wa Wilaya Mbinga, Aziza Mangosongwa alisema, wamepanda miche 20,000 ya kahawa na tayari wameweka mikakati kwa kila shule wanafunzi kupanda miti hasa kwenye yale madarasa ambayo si ya mithiani kupanda mtu mmoja mmoja kila mmoja na wanafatilia.

Kwa upande wake, Kamanda wa Wakala wa Misitu Kanda ya Kusini, Manyisye Mpokigwa alisema mwaka huu wamepanga kupanda miti milioni nne mkoani Ruvuma ikiwemo ya mbao, matunda na kivuli.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live