Katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaosababisha hali ya ukame, mkoa wa Pwani umeweka zuio kwa wafugaji wanaotoka nje ya mkoa huo kuingiza mifugo na ile iliyoingia pasipo kufuata utaratibu iondolewe.
Hayo yamebainishwa jana Jumatatu Novemba 7, 2022 na mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge wakati wa kikao cha wadau wa mazingira na maji kilichoketi mjini Kibaha kwa lengo la kuweka mikakati ya kukabiliana na uharibifu wamazingira.
Mbali na hilo pia amepiga marufuku tabia ya baadhi ya wakulima ya kuchepusha maji kutoka kwenye mito kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwani linaleta athari kubwa.
“Watendaji fanyeni kazi na wananchi washirikisheni, wapeni elimu kísha fanyeni utekelezaji, hivi sasa hali siyo nzuri kimanzingira,” amesema Kunenge.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema ili kufikia suluhisho kuna kila sababu watendaji na viongozi wa ngazi mbalimbali kufanya kazi kwa kuishirikisha jamii pamoja na kuongeza uwajibikaji.
Amesema ingawa Serikali imeendelea kufanya jitihada za kukabiliana na vichocheo vinavyosababisha hali hiyo, ni muhimu kuishirikisha jamii ili iwe mstari wa mbele kulinda vyanzo vya maji.
Aweso amesema kinachotakiwa kufanyika ni kila mmoja kuwajibika kulingana na nafasi yake lakini wananchi pia wanapaswa kuelimishwa ili waendelee kulinda vyanzo vya maji.
Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasa, Jenerali mstaafu, Davis Mwamunyange amesema Taasisi hiyo inategemea zaidi ushirikiano wa wananchi katika kutekeleza majukumu yake, hivyo ni vema watendaji wa chini wakatilia mkazo kuwashirikisha kwa njia mbalimbali.
Naye Kamishina msaidizi wa uhifadhi TFS, kanda ya Masharik, Caroline Malundo amesema ili kuokoa mazingira yanayosabisha ukame hasa kwa wananchi kukata miti kwa matumizi ya mkaa na kuni, kuna kila sababu ya kuongeza kasi ya kuzalisha nishati ya gesi.