Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC:Ondoa watumishi elimu waliokaa miaka 5

D7bf98717067688c7f0df90880411b63 RC:Ondoa watumishi elimu waliokaa miaka 5

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti ameagiza kuondolewa kwa watumishi wa idara ya elimu wilayani hapo, waliodumu kwa zaidi ya miaka mitano.

Amesema hao ndio wanaokwamisha jitihada za ufaulu wilayani hapo.

Mkirikiti alitoa agizo hilo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Solomon Isack.

Kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa inakuja baada ya wilaya hiyo kushika nafasi ya mwisho kimkoa kwa miaka mitatu mfululizo; huku watumishi wa idara hiyo wakishindwa kubuni mbinu mpya za kuongeza ufaulu.

"Nimekuja wilaya hii kama Mkuu wa wilaya hii nikakuta Hanang ni ya mwisho watumishi wa idara hiyo ni wale wale, mwaka wa pili nikiwa hapa tumefeli kama wilaya, tena nikiangalia wataalamu waliopo bado ni wale wale. Mwaka huu tena mmefeli, watu ni wale wale, nasema mkurugenzi ondoa watu hawa," alisema Mkirikiti.

Alisema ili kuhakikisha wanaongeza kiwango cha ufaulu wilayani hapo, bila kuwatoa wataalamu hao wa muda mrefu bado ni tatizo.

Alisema hata wakiwaleta maofisa elimu wengine wapya, bila wataalamu hao wa chini kuondolewa, itakuwa bado ni tatizo.

Alieleza kuwa kinachotakiwa ni kuwaondoa na kuleta wengine wapya, watakaoisaidia wilaya hiyo kuongeza ufaulu na kuacha kushika nafasi ya mwisho kimkoa kila mara.

Mkirikiti aliwataka pia kukamilisha miundombinu ya madarasa ili wanafunzi waliofaulu waweze kuingia darasani na kuanza masomo yao.

"Mwanzoni mpaka naondoka hapa tulikuwa na upungufu wa madarasa 78, tukayapunguza yakafika 15 sasa kama yameongezeka, nendeni hivyo hivyo msijipunguzie maana kule mkoani nikiwaambia nileteeni upungufu wa madarasa mnaniambia hamna upungufu wa madarasa,” alisema.

Alisema wilaya hiyo ina upungufu wa madarasa 14 na kuitaka ijiwekee lengo la kujenga madarasa 30.

“Mnasema madarasa yanatosheleza Hanang ndio sababu mmeendelea kuwa watu wa kufeli, kwa sababu hakuna wa kufaulu madarasa ndio maana yanatosha na kama wangekuwepo kugekuwa na uhitaji," alisema Mkirikiti.

Pia, alimuagiza mkurugenzi kuwaondoa walimu wanaofanya kazi kwa mazoea, kwani nao hao ni tatizo na wakwamishaji wa elimu wilayani hapo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Gharibu Lingo alieleza kuwa watoto wa darasa la saba waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza ni 4,773. Alisema wana upungufu wa madawati 1,837 na madarasa 30. Yote hayo yanatakiwa yapatikane ifikapo Januari mwakani.

Chanzo: habarileo.co.tz