Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC: Njooni tumzike, tumuage rais wetu

336b470d7a10403f2b495db124c8ab28 RC: Njooni tumzike, tumuage rais wetu

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa (RC) wa Geita, Robert Gabriel ametoa mwito kwa wakazi wa Mkoa wa Geita kujitokeza kwa wingi kumuaga, Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17, mwaka huu.

Aidha, ametoa mwito kwa Watanzania kumuombea Rais mpya wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine waliobaki ili taifa liendelee kushikamana, kusonga mbele kwa nguvu na ujasiri, uzalendo na kwa kujiamini. Mwili wa Magufuli utazikwa kesho Chato mkoani Geita.

Baada ya kifo cha Magufuli, Samia aliyekuwa Makamu wa Rais, aliapishwa kuwa rais wa Tanzania kama yalivyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kifo cha rais.

Gabriel ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Geita, alisema leo ndio siku rasmi kwa wananchi wa Mkoa wa Geita kuaga mwili wa marehemu na kutoa heshima zao mwisho, hivyo waitumie vizuri fursa iliyotolewa kwa kujitokeza kwa wingi kumuaga.

Alisema hayo jana katika mazungumzo maalumu kuelezea maendeleo ya maandalizi ya maziko baada ya tukio la mwisho la kuaga mwili wa Hayati Magufuli litakalofanyika kesho katika Uwanja wa Magufuli wilayani Chato.

Mkuu wa mkoa alisema tayari maandalizi yamekamilika kwa ajili ya mazishi na maziko huku usalama ukiwa umeimarishwa katika maeneo yote.

"Tumeshuhudia ulimwengu mzima unamuomboleza, kuna watu hawakuwa wanamfahamu, lakini walimfahamu kupitia kazi zake, kwani mambo ambayo ameyaonesha watu hawajawahi kuamini kwamba yanaweza yakafanywa na Mwafrika; ni lazima tumuage kwa heshima shujaa wetu," alisema.

Aliongeza kuwa, mtihani mkubwa walionao kama viongozi aliowaacha ni kubaki kwenye reli ileile ya uadilifu, utumishi na uwajibikaji katika uongozi.

Alisema kufanyika kwa mambo hayo, kutasaidia kuleta mapinduzi makubwa nchini na kusimamia mifumo yote imara aliyoisimamia na kuilinda kwa nguvu zote.

"Njia pekee ya kumuenzi kiongozi huyu kwetu sisi viongozi na Watanzania kwa jumla, ni kufuata falsafa zake, maelekezo yake, mwelekeo wake na dira yake kama kiongozi aliyekuwa na maono makubwa kwa taifa, Afrika na ulimwengu mzima,” alisema Gabriel.

Akaongeza: "Tukifanya hivyo, tutakuwa tunaidhihirishia dunia kwamba Magufuli hakuwa peke yake; wamezaliwa wengine wengi ili jambo hili tukufu ambalo Mwenyezi Mungu ameliruhusu lipite na taifa letu liendelee kubakia imara na lisitetereke," alisema Gabriel.

Chanzo: www.habarileo.co.tz