Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mwanza atoa siku moja maji yawe yanatoka

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza.  Licha ya Serikali ya awamu ya tano kuweka mkazo katika upatikanaji huduma muhimu kwa jamii ikiwamo afya na maji, bado baadhi ya wakazi wa wilaya ya Ilemela mkoani hapa huduma hizi kwao ni tatizo.

Hali hiyo inadaiwa kuchangiwa na kutokamilika kwa wakati kwa mradi wa maji unaojengwa eneo la Igombe.

Kufuatia hali hiyo, Serikali ya mkoa imetoa muda hadi Machi 31, 2019 kwa mamlaka ya maji na mkandarasi anayejenga mradi huo kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero ya maji kwani Serikali ilishatoa fedha kwa ajili ya mradi huo.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo unaotarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 41,643 katika kata tano za Bugogwa, Sangabuye,  Shibula,  Kahama na Nyamhongolo na kubaini kwamba licha ya muda kumalizika lakini mradi huo bado haujakamilika.

“Serikali ya awamu ya tano itaendelea kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na hiyo ndiyo ajenda yake kuu. Nimetoa hadi Machi 31 mwaka huu (2019) mradi huo uwe umekamilika na maji yanatoka kwa ajili ya wananchi,” Mongella

Kulingana na mhandisi wa maji manispaa ya Ilemela, Anna Mawala, licha ya mapungufu ya mabomba ya kusambaza maji, Serikali kupitia miji iliyopo kwenye maziwa makuu imeleta mradi mwingine mkubwa wa maji ambao tayari umepata mtaalamu mshauri kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi.

“Lengo la Serikali ni kila Mwananchi apate huduma ya maji karibu kabisa na eneo alilopo na ndilo lengo la kumtua mama ndoa kichwani,” Mawala.

Mmoja wa wakazi wa Igombe, Emmanuel Chayonga, alisema pamoja na ukosefu wa maji, umeme pia ni changamoto kwani kuna nguzo za miaka mingi ambazo hazina nyaya.

Kuhusu upatikanaji huduma bora za afya kwa wananchi wa eneo hilo, kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Ilemela, Phinias Elias alisema kuna uhaba wa dawa katika kituo cha afya Karume hususan Vitamin ‘B’ licha ya kuwa ni kati ya dawa 33 muhimu ambazo hazitakiwi kupungua kwenye kituo cha afya.

Aliongeza kuwa kituo hicho cha Karume kina watumishi 42 wakiwemo madaktari tisa na hivyo kupungukiwa na watumishi wanane ambao ni wauguzi ili kufikia jumla ya watumishi 50.

Akijibu hoja za kaimu mganga mkuu, mkuu wa mkoa huo alisema ofisi yake haijapata taarifa yoyote kuhusiana na uhaba wa dawa kwenye hospitali wala zahanati.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz