Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mwanri: Kifo cha Ruge Mutahaba kilinifanya nilie hadharani

46317 Mwaripic RC Mwanri: Kifo cha Ruge Mutahaba kilinifanya nilie hadharani

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amemkumbuka aliyekuwa mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba akisema aliposikia kifo chake alilia hadharani.

Akizungumza leo Jumanne Machi 12, 2019 katika uzinduzi wa jukwaa la mawasiliano ya afya liitwalo Naweza, RC Mwanri amesema marehemu Ruge alishiriki kutoa mchango wake kwa mkoa wa Tabora na kusaidia kupunguza baadhi ya magonjwa hasa ya kuharisha.

Amesema marehemu alipokuja Tabora wakati wa tamasha la fiesta, amesema watu wanapata matatizo ya kuharisha sababu hawanawi mikono.

RC Mwanri amesema jambo hilo lilimshangaza sana na kuamua kuchukua hatua ambapo walibaini sehemu za kutolea huduma ya vinywaji baadhi hazikuwa na vyoo au kama vilikuwepo kuchanganywa na vinywaji au vyakula.

Amesema walichukua hatua ya kuzifungia sehemu ambazo hazikukidhi vigezo vya afya na matokeo yake kuwa chanya.

Mkuu huyo wa mkoa amesema hata shuleni, wanafunzi sasa wananawa mikono kabla na baada ya kula au kwenda na kutoka chooni.

"Namshukuru sana marehemu Ruge kwa ushauri wake mzuri ambao tumeufanyia kazi na sasa matunda tunayaona," amesema.

Jukwaa la Naweza ambalo ni kwa ajili ya watu wazima wenye umri wa miaka 18 hadi 49 na limeratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto, Marcelina Mpandachalo amesema zaidi ya wanawake wajawazito 263  wamefariki dunia mkoani Tabora katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Amesema wajawazito hao wamefariki kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 kwa mkoa mzima wa Tabora.

Mratibu huyo amesema katika kipindi hicho cha miaka mitatu, walijifungua jumla ya wajawazito 282,900. Amesema mwaka 2016 walifariki 95, mwaka juzi walifariki 99 na mwaka jana walifariki 69.

Ametaja baadhi ya sababu za vifo hivyo kuwa ni kutokwa damu nyingi kabla, wakati na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba na uzazi pingamizi.

Amesema ili kupunguza vifo hivyo ni vizuri wajawazito wakapata huduma mapema ikiwa ni pamoja na kuhudhuria kliniki mara nne kabla ya kujifungua.

Amesisitiza pia wanaume kuambatana na wenza wao wanapokwenda kuhudhuria kliniki.

Amebainisha kwamba jitihada kubwa zimefanyika katika kupunguza vifo hivyo mkoani Tabora na jitihada zaidi zinaendelea ili kupunguza vifo hivyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz