Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mtwara azindua soko la madini

61347 Pic+madini

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Katika kuhakikisha wachimbaji wa madini wanakuwa karibu na masoko, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema wataendelea kufungua masoko mengine mkoani humo ili wachimbaji wasihangaike kufuata soko mjini Mtwara ilimradi vigezo vya msingi vya usalama vinazingatiwa.

Akizungumza leo Jumanne, Juni 4, 2019 wakati wa kuzindua soko la madini lililopo mjini Mtwara katika ofisi za madini amesema watafanya hivyo ili kupeleka uratibu wa shughuli hiyo karibu na walipo wachimbaji wa madini au watu wenye madini ili mradi wazingatie vigezo na kamati inasimamiwa na katibu tawala wa mkoa

“Tulianza maandalizi Masasi kwa sababu taarifa tulizo nazo tuna leseni za wachimba dhahabu mbili ambazo ziko hai wilayani Nanyumbu, lakini pia tunawatambua ambao wanamiliki migodi kwa wilaya ya Masasi. Kwa Masasi tulianza utaratibu wa kulifungua soko, sio kwamba taratibu hizo zimesitishwa tutalifungua,” amesema Byakanwa

“Tunataka mchimbaji wa madini Nanyumbu asitoke kote huko kuleta madini yake Mtwara, kote kule alipo vikishazingatiwa vielelezo vya msingi vya kiusalama tutafungua masoko ya madini kadri itakavyoruhusu,” amesema

Naye ofisa madini mkazi mkoa wa Mtwara, Ephraim Mushi amesema kuanzishwa kwa masoko hayo ni kutokana na ukosefu wa sehemu rasmi za kuwezesha wachimbaji wadogo kuuza madini yao na kupeleka kutopata bei stahiki ya thamani ya madini na hata kusababishwa utoroshwaji wa madini.

“Serikali imefanya mabadiliko katika sheria ya kodi kwa kufuta kodi zilizokuwa kero kwa wachimbaji kama kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya zuio,” amesema Mushi

Pia Soma

 

Kwa mujibu wa Mushi mkoa wa Mtwara kwa sasa una leseni 386, leseni 17 za utafiti, leseni moja ya uchimbaji mkubwa, leseni nne za uchimbaji wa kati na leseni 364 za uchimbaji mdogo.

Katibu mkuu wa chama cha wachimbaji madini Mtwara, Abdallah Esmail amesema wanafarijika na ushirikiano wanaoupata kutoka serikalini kwani wameanza kuonja matunda.

“Kilio cha zaidi ya miaka 20 cha kodi zilizokithiri za wazalishaji wa chumvi kilipata utatuzi, tunaahidi tutayatumia masoko na kuyalinda, wachimbaji tutakuwa askari namba moja wa rasilimali madini na tuna wajibu wa kuwavutia wadau wa biashara ya madini ifanyike kihalali Mtwara,” amesema Ismail

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz