Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mtwara aunda kamati kuichunguza Tarura

33813 Pic+mtwara Tanzania Web Photo

Fri, 28 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Kusuasua kwa miradi inayotekelezwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kumefanya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa kuunda kamati za kuchunguza utendaji kazi wake katika Manispaa ya Mtwara Mikindani na halmashauri ya mji Nanyamba.

Amesema haridhishwi na utendaji kazi wa Tarura na baadhi ya barabara zimekuwa hazipitiki na kuwa kero kwa wananchi hasa nyakati za mvua.

Byakanwa ameyasema hayo jana Alhamisi Desemba 27, 2018 katika kikao cha bodi ya barabara na kusema baadhi ya miradi mingine pamoja na kwamba imekuwa ikisuasua lakini wamekuwa wakiitekeleza bila kushirikisha ofisi yake.

“Nataka kupata ripoti ya kina nani mkandarasi amejenga barabara, kwa gharama gani na taratibu zilizotumika kumpata mkandarasi, inafika sehemu wananchi wanapata maneno ya kusema kwa sababu ya watu tuliowaita wataalamu,” amesema Byakanwa.

Amesema kamati iliyoundwa itakwenda katika halmashauri ya Mji Nanyamba kuangalia kama walishakaa na kupitia upya mkataba na kubadili vipengele vyake kuwa barabara iliyokusudiwa kujengwa kwa kiwango cha lami sasa itajengwa kwa kiwango cha changarawe .

“Yote haya yangefanyika tungekuwa kwenye ukurasa mmoja tunaelewana, hatuwezi kumruhusu Tarura akawa mnyama asiyetawalika na kuwa mnyama anayejitawala mwenyewe, kipindi hiki cha mvua ndio mnakwangua barabara ili mje mseme mvua ndio iliyoharibu,” amesema Byakanwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Newala Mjini (CCM), George Mkuchika amesema Tarura inapaswa kushirikiana na halmashauri katika utendaji wake ili kuleta ufanisi katika kazi sambamba na kuwapa mpango kazi wao.

“Wilaya nyingine kama si maelekezo ya Serikali, Tarura walikuwa hawataki shughuli zao zijadiliwe na halmashauri, huwezi kuwatengenezea wao barabara halafu usijadiliwe, hata madiwani wasijue, lazima hata ule mpango wapate mwaka huu unataka kutengeneza barabara hivi na hivi na ushauri utatolewa pale hapana hii barabara haipitiki bora ile,” amesema Mkuchika.

Mratibu wa Tarura mkoa wa Mtwara, Siraji Mbuta amesema changamoto kubwa inayowakumba ni bajeti kidogo inayotengwa kuliko uhalisia ambapo wanapata asilimia 30.

Amesema kamati ya kitaifa ya kupandisha madaraja barabara inapitia mtandao wa barabara za Tarura ili iweze kutoa mgao wa fedha

“Tarura inapata asilimia 30 wakati ina mtandao mkubwa wa barabara, baada ya zoezi la uhakiki formula itabadilika na Tarura itapata fedha za kutosha kuweza kuhudumia barabara,”amesema Mbuta.



Chanzo: mwananchi.co.tz