Mtwara. Imeelezwa baadhi ya watendaji na wasimamizi wa sheria wamekuwa wakikwamisha watendaji wa sekta binafsi kutokana na kutokufanya uamuzi kwa wakati licha ya mambo kuwa wazi katika sheria.
Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Mtwara nchini Tanzania, Gelasius Byakanwa wakati akizindua baraza la biashara la mkoa wa Mtwara leo Jumamosi Septemba 7, 2019 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma kwa kutumia jukwaa la majadiliano na mashauriano ili kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara.
“Tatizo kubwa lililopo kwa sisi wasimamizi wa sheria na taratibu ni kutofanya uamuzi, mnakwama sana nyie upande wa pili (sekta binafsi) kwa sababu sisi hatuwezi kuamua na wakati mwingine mambo yako wazi kwa sheria yaani kama umeshapewa na mandate (mamlaka) fanya hiki kitu halafu bureaucracy (urasimu) inatoka wapi unaamua mtu mwingine anamjibu kwa nini unanisumbua sana na simu yako..hao ndio watendaji,” amesema Byakanwa
Amesema watendaji wa umma kama watasimamia sheria hizo wakijua ni wao ni sekta binafsi tarajiwa wanaweza kuleta mabadiliko makubwa pengine kwa kutumia sheria ambazo zipo.
“Tunapokutana na kujadiliana na kuzisema changamoto ambazo ziko kwenye sheria na sera ili sisi wasimamizi tuone ni wapi ambapo tunaweza kuboresha na mazingira ya ufanyaji biashara yakawa mepesi na rahisi.”
Pia Soma
- Walichokisema Mbowe, Maalim Seif kushambuliwa Tundu Lissu
- VIDEO: Haya ndio madhara ya chupa za plastiki
- VIDEO: Meno ya Tembo yalifukiwa humu
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha wafanya biashara ,viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoa wa Mtwara, Said Swallah amesema uundwaji wa mabaraza ngazi ya wilaya ya mkoa ni agizo la serikali agizo linalotokana na kuanzishwa baraza la Taifa la biashara kupitia waraka wa Rais namba moja mwaka 2001 na kuchapishwa katika gazeti la serikali.
“Moja ya majukumu ya baraza ni kushughulikia kero, migogoro na changamoto katika ufanyaji biashara na uwekezaji na ndio maana Serikali baada ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu kero na changamoto zinazoathiri mazingira ya biashara na uwekezaji kutokuwa rafiki imepisha mpango kazi wa uboreshaji mazingira ya biashara na uwekezaji (blue print) ambao unapaswa kujadiliwa kwa pamoja kati ya sekta ya umma na binafsi,” amesema Swallah